Wizara ya Madini kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) imekabidhi eneo la ujenzi wa Kituo cha Umahiri Bariadi Mkoani Simiyu kwa Mkandarasi wa ujenzi huo SUMA JKT ambao unaotarajiwa kuanza mwezi huu wa Julai 2018.
Makabidhiano hayo yamefanyika jana Mjini Bariadi Mkoani Simiyu na kushuhudiwa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka, mara baada ya timu ya wataalam wa Wizara ya Madini na SUMA JKT kutembelea eneo la ujenzi lililopo Nyaumata Mjini Bariadi.
Akizungumzia kituo hicho Afisa Madini Mkoa wa Simiyu, Bw. Fabian Mshai amesema “Kituo hiki ni Jengo la Ofisi ambalo litakuwa na kumbi za kutolea mafunzo mbalimbali yahusianayo na uchimbaji wa madini unaozingatia kanuni za afya, usalama, uchambuzi wa madini na uhifadhi wa mazingira kwa wachimbaji wadogo ili uchimbaji uwe wenye tija”
Mshai ameongeza Kituo hiki cha Umahiri Bariadi kitajengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.3 na Kampuni ya Ujenzi ya SUMA JKT na kusimamiwa na Kampuni ya Sky Actate Consultants.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kuamua kujenga Kituo hicho kwa kuwa mkoa huo ni mpya na unahitaji majengo mengi, hivyo amaesema ujenzi huo utajibu mahitaji ya mkoa katika kuwasaidia wachimbaji wadogo kuondokana na uchimbaji wa kienyeji na kwenda kwenye uchimbaji wa kisasa
"Wachimbaji wetu wadogo wamekuwa wakifanya shughuli zao kienyeji lakini uwepo wa kituo hiki utajibu mahitaji yao kwa sababu kitakuwa ni sehemu sahihi ya wao kupata elimu juu ya uchimbaji bora, wataalam wa madini watakuwa karibu kwa kuwa ukamilishaji wa kituo hiki utaenda sambamba na uwepo wa rasilimaliwatu" alisema Mtaka.
“ Sisi kama mkoa tuna faida ya uwepo wa rasilimali madini tuna nikeli, shaba, dhahabu, cobalt, tuna chumvi katika wilaya ya Meatu lakini pia tuna madini ya ujenzi kama kokoto, mchanga na mengine, hivyo uwepo wa kituo cha umahiri kutasaidia wachimbaji kufanya kazi zao katika utaalam ili uchimbaji ufanyike kwa ufanisi na uwe na tija” alisema.
Ameongeza kuwa uwepo wa kituo hicho pia utachangia kuboresha mazingira ya utendaji kazi ndani ya mkoa tofauti na ilivyo sasa, ambapo watumishi hao wanatumia majengo ya kukodi ambayo wakati mwingine hayakidhi mahitaji yao.
Amesema kuwepo kwa kituo hicho pia kutasaidia kufikia lengo la Serikali la kuhakikisha Sekta ya Madini inakuwa moja ya vyanzo vikubwa vya mapato kwa kuwekeza utaalam wa rasilimali watu, majengo, upimaji na utaalam mbalimbali wa kusaidia wachimbaji wadogo; hivyo akasisitiza SUMA JKT kukamilisha ujenzi wa kituo hicho kwa wakati.
Naye Luteni Kanali Petro Ngata Meneja wa SUMA JKT Kanda ya Ziwa amemhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka kuwa kazi ya ujenzi wa Kituo cha Umahiri Bariadi itafanyika kwa wakati.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/07/wizara-ya-madini-yakabidhi-eneo-la.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa