Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda na Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Festo Dugange wameshiriki kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Simiyu (RCC), ambapo walitumia fursa hiyo kuwasilisha masuala ya kilimo na afya kwa viongozi wa chama na serikali, wakuu wa Taasisi za Umma na binafsi, viongozi wa Dini na wadau wengine wa maendeleo.
Akizungumzia kuhusu kilimo cha zao la pamba katika kikao hicho kilichofanyika Desemba 15, 2020 Mjini Bariadi Prof. Adolf Mkenda amesema Wizara ya kilimo itafanya mapitio ya mifumo mbalimbali ya kitaasisi ili kuongeza tija katika uzalishaji wa pamba kufikia lengo la kuzalisha tani milioni moja ndani ya miaka mitano ijayo.
Miongoni mwa mifumo aliyoibainisha Profesa Mkenda ni pamoja na mfumo wa kushughulikia pembejeo za kilimo huku akibainisha kuwa Wizara yake inaendelea kufanya uchunguzi ili kuona kama uwezekano wa kuzalisha viuatilifu nchini ili kupunguza uagizaji wa viuatilifu kutoka nje ya nchi na kuweza kudhibiti ubora wa viuatilifu hivyo.
“ Katika kufikia tija kwenye zao la pamba pia tunapitia upya na kwa haraka sana mfumo mzima wa kitaasisi wa kuzalisha na kugawa mbegu za pamba, utaratibu mpya hautakuwa umekamilika kwa kipindi hiki cha msimu huu, lakini tumekusudia na tumekubaliana tutafanya mapitio ili wakulima wapate mbegu bora kwa wakati,” alisema Profesa Mkenda.
Awali Kabla ya kuzungumza katika kikao hicho Prof. Mkenda, wajumbe wa Kikao cha RCC waliwasilisha changamoto mbalimbali katika kilimo cha pamba ikiwa ni pamoja na tatizo la upungufu wa mbegu na mbegu kutowafikia wananchi kwa wakati.
“Kumekuwa na changamoto ya upungufu wa mbegu kwa wakulima, ninashauri ili mbegu ziwafikie wakulima wote na kwa wakati, makampuni yanayozalisha mbegu yazipeleke kwa Mkurugenzi ambaye ndiye mwenye wataalam wa kilimo wanaofahamu idadi ya wakulima na ukubwa wa maeneo wanayolima,” alisema Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Benson Kilangi.
“Pamoja na kutatua changamoto ya pamba, tunaomba serikali iajiri maafisa ugani ili wananchi waweze kupata huduma za ugani na kuzalisha kwa tija,tutakapozalisha kwa tija tutapata mavuno mengi na mkulima atanufaika pamba yake, suluhisho la bei ya pamba ni kujenga kiwanda cha nguo mkoani Simiyu,” Mhe. Esther Midimu Mbunge Viti Maalum.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Festo Dugange ametoa rai kwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya ya Busega, Bariadi na Itilima kuanza kununua vifaa tiba kwenye Hospitali za Wilaya zilizojengwa kwa kutumia mapato ya ndani huku akibainisha kuwa Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa kila hospitali kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba.
Dkt. Dugange pia amesema katika miaka mitano ijayo Serikali ina mpango wa kujenga vituo vya kutolea huduma za afya takribani 655 huku akifafanua kuwa itaanza na ukamilishaji wa maboma yaliyojengwa na kwa nguvu za wananchi na kuomba Halmashauri kuweka mpango wa kuanza kukamilisha maboma hayo.
Dkt.Dugange amesisitiza juu ya umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa mifumo ya ukusanyaji mapato katika vituo vya kutolea huduma za afya, ambapo amebainisha kuwa makusanyo yakiwa mazuri yatazipunguzia Halmashauri mzigo wa utegemezi kwa Serikali Kuu na wadau mbalimbali wa afya na kuwezesha vituo hivyo kujiendesha ikiwa ni pamoja na kuwa na uwezo wa kununua dawa.
Akifunga kikao cha RRC Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewashukuru viongozi hao kushiriki katika kikao hicho, huku akitoa wito kwa viongozi wote wa Mkoa huo kuifanya elimu kuwa ajenda ya kudumu ya mkoa na ujenzi wa vyumba vya madarasa kuwa ni kipaumbele chao cha kwanza ili kila mwanafunzi aliyefaulu aweze kwenda shule.
MWISHO.
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2020/12/waziri-wa-kilimo-prof-mkenda-naibu.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa