Serikali kupitia waziri wa kilimo Japhet Hasunga imezindua Bima ya Kilimo inayokinga mazao ya mkulima yanapokuwa shambani dhidi ya ukame, magonjwa ,wadudu waharibifu , mvua zilizozidi, moto, uharibifu unaoweza kusababishwa na wanyapori, pamoja na mvua ya mawe.
Akizundua bima hiyo Hasunga amesema kuwa wameamua kuanza na kipaumbele katika zao la pamba ambalo huzalishwa kwa wingi Mkoani hapa lengo likiwa ni kuwainua wakulima wenye vipato vya chini sambamba na kuwasaidia kupata msaada pindi wanapopatwa na majanga ambapo bima hiyo inatarajiwa kuzinduliwa kwenye mazao mengine ya kimkakati.
Aidha waziri Hasunga amewataka wakulima walio katika vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) kuhakikisha wanajiunga na bima ya mazao itakayowasaidia kukuza uchumi wao na kuongeza kuwa idadi ya vyama vya ushirika katika mazao yote imeongezeka na kufikia 11,331 ambapo kiwango cha ukaguzi wa vyama hivyo ni 70% na kuisisitiza Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuongeza kasi ya ukaguzi ili ifikie 100%.
“Bima hiyo ya mazao itamsadia mkulima kuepukana na majanga mbalimbali na kwamba tumeamua kulipa kipaumbele zao la pamba na baada ya hapa tutaenda Kagera kuzindua bima kwenye zao la kahawa na serikali imelenga kuongeza kuwainua wakulima ili waweze kuchangia katika kukuza pato la Taifa”alisema waziri Hasunga
Ameongeza kuwa wakati umefika wa kuwachukulia hatua za kisheria waliohujumu vyama vya ushirika awali huku akiwataka waliopewa majukumu kwenye AMCOS kuwa wachapakazi, waadilifu na waaminifu katika utendaji kazi wao.
“nitoe tamko kuwa viongozi wote wa vyama vya ushirika ambao wanawafanya ubadhilifu na kuihujumu serikali ni lazima wachukuliwe hatua za kisheria na pia ni vyema sasa sheria na miongozo iliyopo ibadilishwe ili iweze kuendana na kasi ya ushirika uliopo” alisema
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima ya Taifa (NIC) dokta Elirehema Doriye amesema kuwa shirika hilo linatarajia kutoa bima ya mazao kwa wakulima wote nchini huku akiwashauri wakulima kukata bima ili kuepukana na changamoto.
Aidha ameongeza kuwa bima hiyo itamsaidia mkulima kuweza kukopesheka kwenye mabenki kwani tayari mkulima atakuwa na kinga hivyo kutoa mazao yatakayochangia pato lake na Taifa kwa ujumla huku akiongeza kuwa shirika hilo linalomilikiwa na serikali kwa asilimia mia moja 100% likiwafikia wakulima wote na kwa kuanzia wataanza na wakulima wadogo.
Pamoja na hayo ameongeza kuwa bima hiyo ina manufaa makubwa kwa mkulima na itamkomboa kutoka katika kilimo kidogo na kwenda kikubwa kitakachomuwezesha kuwekeza katika kilimo cha kisasa bila kuwa na hofu ya kupoteza mtaji aliowekeza shambani ikiwa sekta kilimo imeajiri zaidi ya 75% ya Watanzania.
Kwa upande wake Kamishina wa Bima hapa nchini Dkt. Mussa Juma ameeleza kuwa lengo la bima hiyo ni kusaidia kuinua kipato cha watu wenye kipato cha chini ili waweze kuchangia katika ukuzaji wa uchumi wa nchi .
Mbali na hayo amesema kuwa uchumi wa nchi unategemea sekta mbalimbali ambazo ni kama kilimo, uvuvi, mifugo, madini na ili kuwa na viwanda ambavyo vinaweza kusaidia kukuza uchumi wa nchi lazma kuwe na namna ya kudhibiti majanga.
Hata hivyo ameongeza kuwa bima ambazo zinahusu watu wengi hasa wenye kipato cha chini mamlaka imeona iweze kuwafikia kwa namna moja nyingine.
Awali akimkaribisha waziri Hasunga mkuu wa mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka amesema kuwa mkoa umejiandaa kikamilifu kusaidiana na NIC katika kuhakikisha zaidi ya wakulima 100,000 wa pamba waliosajiliwa wanapata bima ya mazao.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/08/waziri-hasunga-azindua-bima-ya-mazao.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa