Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera ,Bunge Kazi,Vijana ,Ajira na Walemavu Mhe. Anthony Mavunde ametoa wito kwa Wazazi nchini kuwalea watoto wao katika maadili mema ili kuwaepusha na matumizi ya dawa za kulevya na Maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi.
Ushauri huo ameutoa wakati akifungua makambi ya siku saba ya Kanisa la Waadventisa Wasabato mkoani SIMIYU, katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Mavunde amesema malezi ya watoto ni jambo muhimu sana hasa katika kizazi cha hivyo watoto wakikosa malezi bora katika umri walio nao ni rahisi kutumbukia katika makundi yasiyofaa yakiwemo ya matumizi ya dawa za kulevya na hivyo kukosa nguvu kazi ya Taifa.
“Kwa mujibu wa takwimu Tanzani kila siku watu 200 wanapat maambukizi mapya ya VVU katika watu 200 watu 80 ni vijana katika hao vijana 80 asilimia 80 ni watoto wa kike, hivyo tuendelee kuelemisha na kuliandaa hili kundi kubwa la Vijana katika malezi bora ili wawe nguvu kazi ya kuleta tija katika Taifa letu” alisema.
Ameongeza kuwa ili watu waweze kuondokana na umaskini ni lazima wafanye kazi hivyo akatoa wito kwa Viongozi, waumini wa Kanisa la Waadventisa Wasabato na wananchi wote kufanya kazi kwa staha, uadilifu na malengo ili waweze kufanikiwa kiuchumi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema makambi hayo ni sehemu ya Maandalizi ya Mkutano mkubwa wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali Waadventista Wasabato (ATAPE) unatarajiwa kufanyika mwaka 2019 mkoani humo.
Aidha, Mtaka alitumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi kuwa mwaka 2019 kutakuwa na matukio makubwa matatu ambayo yataitambulisha Simiyu ambayo ni mkutano huo wa ATAPE, Mkutano wa Madaktari wa Nchi nzima na Maonesho ya Nanenane ya Kimataifa.
Katika hatua nyingine amewahimiza wananchi kujifunza masuala ya Ujasiriamali na kuwakaribisha katika Maonesho ya Viwanda Vidogo SIDO yatakayofanyika Kitaifa mwaka huu 2018 kuanzia tarehe 24 hadi 28 Oktoba, 2018 katika Viwanja vya Nyakabindi.
Awali akitoa somo kuhusu masuala ya Ujasiriamali, Mchungaji Joshua Njuguna aliwasisitiza waumini wote kuwa siyo mpango wa Mungu mtu yeyote awe maskini , akawaasa kufanya kazi ili kuutafuta utajiri hivyo akawataka wazitafute fursa za kupata utajiri na kufanya kazi kwa bidii.
Pia Naibu Waziri Mavunde ameahidi kuchangia jumla ya mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya kuwaunga mkono Waumini hao katika ujenzi wa Hospitali ya Kanisa katika eneo la Pasiasi jijini Mwanza.
Ufunguzi wa makambi umehudhuriwa na waumini mbalimbali kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini, lengo likiwa ni kujifunza neno la Mungu, kutoa elimu ya ujasiriamali, mafunzo ya ndoa na malezi ya watoto na kuliombea Taifa.
MWISHO
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa