Halmashauri ya wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu imetakiwa kutoa kipaumbele kwa wawekezaji wazawa pindi wanapogawa maeneo ya uwekezaji wa viwanda ili kusaidia kukuza ajira na uchumi ndani na nje ya Mkoa, ambapo jumla ya ekari 1000 zimeshatengwa kwa ajili yauwekezaji.
Wito huo umetolewa leo na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2017 Amour Hamad Amour wakati wa kukagua na kukabidhi hati ya eneo la uwekezaji wa viwanda kwa Mkurugenzi wa Halmashauri lililopo katika kata ya Nyalikungu Wilaya ya Maswa
.
Kiongozi huyo amepongeza Uongozi wa Wilaya ya Maswa kwa kutekeleza agizo la Serikali la kutenga eneo la uwekezaji na kusema kuwa ni vema wazawa wakapewa kipaumbele kwa kupatiwa maeneo hayo, ili waanze ujenzi wa viwanda mbalimbali vitakavyokuza ajira, kuchangia pato la Halmashauri, pato la mwananchi mmoja mmoja na uchumi wa Nchi kwa ujumla.
"Nashauri Halmashauri kutoa kipaumbele kwa wazawa kwa kuwapatia maeneo hayo ya viwanda ili wafanye shughuli za kimaendeleo ambazo zitagusa moja kwa moja maisha ya Wananchi wa Wilaya ya Maswa, mkoa wa Simiyu na Taifa kwa ujumla ikiwa ni pamoja suala la ajira kwa vijana ....Alisema.
Pamoja na kuwapa kipaumbele wazawa Ndg. Amour ameutaka uongozi wa Wilaya ya Maswa kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wageni na kutoa maeneo kwa wote watakaokidhi masharti ya kuwekeza na kujenga viwanda kwa mujibu wa sheria za nchi.
Aidha Amour ameishauri Halmashauri hiyo kuanzishwa viwanda ambavyo vitayaongezea thamani mazao na kutoa bidhaa zitakazoingia sokoni moja kwa moja, badala ya kung'ang'ana viwanda vinavyoandaa malighafi zitakazotumiwa na viwanda vilivyo nje ya nchi; kama ilivyo kwa viwana vingi vya pamba huandaa pamba inayoenda kuzalisha nguo nje ya nchi.
Pia amefurahishwa na kuupongeza uongozi mzima wa Halmashauri hiyo kwa jitihada wanazozifanya za kuanzisha viwanda vinavyoiongezea halmashauri mapato kikiwemo kiwanda cha Chaki, sambamba na kuhakikisha wanaendana na kasi ya Mhe Rais ya kuwa na Tanzania ya viwanda .
Naye Afisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa John Nkoko amesema kuwa tayari wameshatenga ekari 1000 kwa ajiri ya eneo la viwanda na tayari eneo la ekari 315.64 limeshaandaliwa michoro ya mipango miji.
Nkoko amesema kuwa lengo la Halmashauri yao kutenga eneo hilo ni kuhakikisha wanatengeneza fursa ya ajira kwa wananchi wao pamoja na kukuza uchumi wao wa ndani na nje ya Mkoa .
Sambamba na hilo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Maswa Dk Fredrick Sagamiko alisema Wilaya yake itahakikisha inapambana kuwa na uchumi wa kati kwa kuanzisha viwanda mbalimbali ambapo mpaka sasa wameanza ujenzi mpya wa kiwanda kikubwa cha chaki ambacho kitakuwa cha kwanza Afrika Mashariki kwa kuwa na teknolojia mpya.
Mwenge wa Uhuru ukiwa Wilayani Maswa umeweka mawe ya mingi, kuzindua, kufungua na kuona miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya Viwanda, Afya, Elimu, Kilimo, Utawala Bora,Maendeleo ya Jamii,Ardhi Maliasili na Mazingira.
Akitoa Ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika maeneo mbalimbali ya miradi Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru amewaasa wananchi kufanya kazi kwa bidii, kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli katika kulinda rasilimali za nchi pamoja na kupambana na rushwa, dawa za kulevya, malaria na UKIMWI.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa