Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye Ulemavu, Mhe.Ummy Nderiananga amewataka watu wenye ulemavu nchini kujitokeza kuchukua mikopo inayotolewa na halmashauri bila riba kutoka katika asilimia mbili ya mapato ya ndani ili waweze kujipatia kipato na kuondokana na adha ya kutumikishwa kama omba omba.
Mhe. Nderiananga ametoa wito huo jana Januari 29, Mjini Bariadi wakati alipokutana na kuzungumza na viongozi wa makundi mbalimbali ya watu wenye ulemavu akiwa katika ziara yake ya siku moja mkoani Simiyu, iliyolenga kufanya ufuatiliaji na uhamasishaji wa masuala ya watu wenye ulemavu..
" Licha ya baadhi ya Halmashauri kufanya vizuri katika kutenga fedha kwa ajili ya watu wenye ulemavu, kuna taarifa kuwa baadhi yenu mmekuwa waoga kukopa fedha zinazotengwa kwa ajili yenu, nitoe rai kwenu tumieni fursa hiyo kopeni ili mpate mitaji ya kuwasaidia kufanya shughuli za kuwaingizia kipato, fedha hizi ni kwa ajili yenu na Serikali imefanya kazi kubwa sana ili mpate fedha hizi,” alisema Nderiananga.
Katika hatua nyingine Nderiananga amewaasa watu wenye ulemavu wanaochukua mikopo hiyo kurejesha kwa wakati kwa mujibu wa miongozo na taratibu za utoaji wa mikopo hiyo ili kutoa fursa kwa kila mmoja anayehitaji mikopo hiyo kuipata kwa wakati.
“Natoa wito kwa watu wenye ulemavu ambao mmekuwa mkikopeshwa fedha itokanayo na asilimia mbili ya mapato ya ndani ya halmashauri kurejesha nawaomba msile, mkila mtafanya watu wenye ulemavu wasiaminike,” alisema Nderiananga
Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu wa viungo (CHAWATA) Mkoa wa Simiyu, Bw Gera Makasi ameomba Viongozi na wataalam kutoka Serikalini waendelee kutoa elimu juu ya mikopo hiyo ili watu wenye ulemavu wapate uelewa mpana juu ya namna mikopo hiyo inavyotolewa, inavyorejeshwa na namna sahihi ya kuitumia kwa manufaa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga amesema Mkoa wa Simiyu unawajali sana watu wenye ulemavu huku akibainisha kuwa Simiyu imejipanga kuanzisha namna ya tofauti (unique model) ya utoaji wa mikopo kwa watu wenye ulemavu, wanawake na vijana ili mikopo itolewayo kutoka katika asilimia kumi ya mapato ya Halmashauri iwe na tija kwa makundi lengwa ( watu wenye ulemavu asilimia mbili, vijana asilimia nne na wanawake asilimia nne)
Akitoa taarifa ya mkoa kwa Naibu Waziri, Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Simiyu, Bw. Ekwabi Mujungu amesema watu wenye uemavu mkoani hapa wamekuwa wakishirikishwa katika shughuli za kijamii na uhamasishaji unaendelea kufanyika ili waweze kuunda vikundi kurahisisha upatikanaji wa mikopo, ambapo mpaka sasa takribani vikundi 45 vya watu wenye ulemavu vimeshaundwa.
Aidha , Mujungu ameongeza kuwa katika bajeti ya mwaka 2020/2021 kiasi cha shilingi milioni mia mbili na laki sita kimetengwa katika halmashauri zote sita za mkoa wa Simiyu (Bariadi Mjini, Bariadi Vijijini, Busega, Itilima, Maswa na Meatu) kwa ajili ya kutoa mikopo kwa watu wenye ulemavu.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2021/01/watu-wenye-ulemavu-watakiwa.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa