Wastaafu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu wamewaasa watumishi wa umma kumtanguliza Mungu, kuwa waadilifu na kujituma ili waweze kutimiza wajibu wao sawa sawa kwa maslahi yao binafsi na Taifa kwa ujumla.
Hayo yamebainishwa na Bw. Elias Kasuka ambaye kwa sasa amestaafu utumishi wa umma akiwa kama Afisa Kilimo Mkuu baada ya kutumika kwa miaka 35 na Bw. Godfrey Machumu ambaye kwa sasa amestaafu utumishi wa umma akiwa kama Mhasibu Mkuu baada ya kutumika kwa miaka 37 katika Hafla fupi ya kuwapongeza wastaafu hao wa mwaka 2019/2020 iliyofanyika Agosti 28, 2020 Mjini Bariadi.
“Katika Utumishi wa Umma hampashwi kukata tamaa, binafsi nimeanzia mbali nikajiendeleza sikujali umri wangu, kikubwa ni kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika kazi zenu mtafanikiwa tu,” alisema Bw. Godfrey Machumu.
“Siri kubwa ya kufikia mpaka kustaafu kwangu ni kufanya kazi kwa bidii na uadilifu, nilifanya kazi bila kusukumwa mfano mzuri ni kwa namna nilivyoshiriki kuandaa Maonesho ya nanenane mwaka 2018 na 2019 ; pia nawashauri mheshimu wakubwa kwa wadogo,” alisema Bw. Elias Kasuka.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi.Miriam Mmbaga amewapongeza wastaafu hao kwa utumishi uliotukuka mpaka kufikia kustaafu huku akitoa wito kwa watumishi wengine kuiga mema waliyojifunza kupitia utumishi wa wastaafu hao ikiwa ni pamoja na kuona umuhimu wa kujiendeleza kielimu wakiwa kazini na kujiendeleza kimaisha.
Katika hatua nyingine Bi. Mmbaga amewaasa watumishi kuishi na watu wote vizuri huku akisisitiza umuhimu wa kuacha alama katika kazi zao wanazofanya ili hata watakapo staafu wakumbukwe kwa alama walizoacha kwenye maeneo waliyofanyia kazi.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2020/08/wastaafu-wawaasa-watumishi-wa-umma.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa