Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2017 Ndg. Amour Hamad Amour ametoa wito kwa wananchi kupenda na kuthamini bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.
Amour ametoa wito huo wakati alipokuwa akitoa ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mara baada ya kuweka jiwe la Msingi Mradi wa kiwanda cha kuongeza thamani ya mazao Kilimo cha BUSEGA MAZAO LIMITED katika kijiji cha Mwanangi wilayani Busega.
Amesema wananchi watakapotumia bidhaa zinazozalishwa hapa nchini watasaidia kuongeza uzalishaji kutokana na kuwepo kwa soko la uhakika kwa viwanda na hatimaye kuongeza uchumi wa nchi.
Ameongeza kuwa wawekezaji wanapaswa kuzalisha bidhaa bora ambazo zitakidhi vigezo vya kiushindani sawa sawa na zile zinazotoka nje ya nchi ili kupunguza uingizwaji wa bidhaa za nje na kulifanya Taifa kuongeza pato lake.
“.....bidhaa ambazo zinazotoka nje zinapoingia hapa ndani zinakuwa na bei ndogo kuliko zinazozalishwa hapa nchini, ni kwa sababu bado hatujajipanga kuzalisha kiushindani, sasa tuzalishe bidhaa zenye ushindani ili kuweza kuua soko la bidhaa ambazo zinatoka nje tuweze kukuza uchumi wa Taifa letu” alisema.
Aidha, amesema mwekezaji wa kiwanda cha BUSEGA MAZAO LIMITED atakapoanza uzalishaji atoe kipaumbele cha ajira kwa wananchi wa wilaya ya Busega na ahakikishe wanafanya kazi katika hali ya usalama na kupewa haki na maslahi yao kama inavyostahili.
Kiongozi huyo wa Mwenge wa Uhuru 2017 pia amewataka wakazi wa Wilaya ya Busega na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla kuhakikisha kuwa wanazalisha kwa wingi mazao yote yanayotakiwa katika kiwanda hicho ukiwepo mpunga na mahindi kwa kuwa kitatoa soko la uhakika na kupelekea ongezeko la pato la mtu mmoja mmoja.
Akisoma taarifa ya mradi wa kiwanda hicho,Ndg. Lazaro Japhet kutoka BUSAGA MAZAO LIMITED amesema Kiwanda hicho kitawasaidia wakulima kupata soko, kuhifadhi na kuongeza mazao yao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe.Tano Mwera amesema Serikali wilayani humo iko tayari kushirikiana na wawekezaji ambao watakuwa tayari kuwekeza katika wilaya hiyo.
Sambamba na hayo Ndg.Amour Hamad Amour amewataka wananchi kufanya kazi kwa bidii, kulinda rasilimali za nchi na kuendelea kupambana na rushwa, dawa za kulevya, malaria na UKIMWI ili kuweza kufikia Tanzania ya Uchumi wa Kati.
Akizungumza na wananchi na wanafunzi katika Shule ya Sekondari Mkula Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2017 amesisitiza wanafunzi wa shule za sekondari kuwa na Klabu za wapinga rushwa, mapambano dhidi ya dawa za kulevya, malaria na UKIMWI ili waweze kufikia malengo yao.
Mwenge wa Uhuru ukiwa Wilayani Busega umepitia jumla ya miradi 9 katika sekta ya Elimu, Afya, Maji,Utawala Bora, Viwanda na Maendeleo ya jamii, yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.5.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa