Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt. Festo Dugange ametoa wito kwa wananchi mkoani Simiyu kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi na kuacha ulaji usiofaa kwa kuacha kutumia vyakula vyenye sukari, mafuta na chumvi nyingi na nafaka zilizokobolewa kwa lengo la kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo kisukari, shinikizo la juu la damu na saratani.
Dkt Dugange ameyasema hayo Novemba 22, 2019 wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya kudhibiti na kuzuia magonjwa yasiyoambukiza, ambayo ilizinduliwa rasmi kimkoa Novemba 22, 2019 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
“ Asilimia 43 ya wagonjwa wanaotibiwa katika vituo vya kutolea huduma za afya wana matatizo yanayotokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kutofanya mazoezi kunachangia kwa asilimia 60 magonjwa yasiyoambukiza, hivyo ni vema wananchi wakafanya mazoezi na kuepuka ulaji usiofaa ili kudhibiti magonjwa haya,” alisema Dkt. Dugange.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amewataka watumishi wa idara ya afya mkoani hapa, kuwafikishia wananchi elimu ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza na kutoa ushauri kwa mtu mmoja mmoja kuhusu umuhimu wa kufanya mazoezi, lishe bora na madhara ya kutumia vilevi kupita kiasi.
Aidha, Sagini amesisitiza wataalam wa afya kuelimisha jamii namna ya kutambua magonjwa yasiyoambukiza kupitia upimaji na kufuatilia watu wenye magonjwa sugu yasiyoambukiza.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga amesema atashirikiana na viongozi wengine kusimamia ufanyaji wa mazoezi ya viungo ikiwemo utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan la kufanya mazoezi Jumamosi ya pili ya kila mwezi ili kuwahamasisha wananchi kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza.
“Tutakachokifanya sasa hivi ni kugawa vituo vya mazoezi ya mara kwa mara kulingana na kanda kwa kuwa mji unakuwa, lakini pia tutaweka viongozi kwa kila kanda, ili kila inapofika Jumamosi ya pili mwezi viongozi wanakuja na watu wao tunajumuika pamoja katika mazoezi,”alisema Kiswaga.
Kwa upande wao watumishi walioshiriki katika mazoezi hayo wamewashukuru viongozi wa Mkoa kwa kuhamasisha watumishi na wananchi kushiriki mazoezi haya, kwa sababu wanatumia muda mwingi kazini wakiwa wamekaa hali inayoweza kuchangia wao kupata magonjwa yasiyoambukiza, hivyo wakaomba utaratibu huo uwe endelevu na waahihidi kushiriki kila wakati ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
“Watumishi wengi tumekuwa tukijihusisha zaidi na shughuli zetu za kikazi tunasahau na wakati mwingine tunashindwa kufanya mazoezi ambayo ni muhimu kwa afya zetu na ufanisi wa kazi zetu, ninashukuru viongozi wetu kuandaa na kufanikisha zoezi hili na sisi kama watumishi tunaahidi kuwa suala hili litakuwa endelevu,” alisema Marko Igenge mtumishi idara ya afya.
Kampeni ya kudhibiti na kuzuia magonjwa ilizinduliwa rasmi kimkoa Novemba 22, 2019 ikiwahusisha viongozi, watumishi wa Taasisi za Umma na binafsi pamoja na wananchi, ambapo utaratibu wa kufanya mazoezi ya viungo utaendelea kufanyika kila Jumamosi ya pili katika kila mwezi.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/11/wananchi-simiyu-washauriwa-kufanya.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa