Wananchi wa Kijiji cha Mwasubuya wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu wamesema Mradi wa Umwagiliaji wa Mwasubuya wenye ekari 514 utawasaidia kubadili maisha yao kiuchumi kwa kuwa wanatarajia kuongeza mavuno kutokana na kuanza kutumia zana za kilimo za kisasa katika uzalishaji kuanzia hatua ya kuandaa mashamba hadi kuvuna.
Wananchi hao wameyasema hayo baada ya makabidhiano ya zana za kilimo za kisasa zitakazotumika kuanzia hatua ya kuandaa mashamba mpaka kuvuna, kutoka Kampuni ya Agricom kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi ambayo imewadhamini wananchi walio katika mradi wa Umwagiliaji wa Mwasubuya, yaliyofanyika katika eneo la Mradi Kijiji cha Mwasubuya, Septemba 03, 2018.
Wamesema pamoja na kuongeza uzalishaji kutokana na uwepo wa maji ya uhakika ya Bwawa la Mwasubuya na matumizi ya zana bora, mradi huo ambao utajikita zaidi katika kilimo cha mpunga pia utawawezesha wananchi na hasa vijana kujiajiri kupitia kilimo cha mboga mboga, hatimaye kukuza kipato chao na Taifa kwa ujumla.
“Tumefurahi sana kupata mradi wa umwagiliaji, hii ni ajira kwetu hasa sisi vijana wenye nguvu, nina imani tukiutumia mradi huu vizuri utatubadilisha sisi kiuchumi kwa sababu mashine za kisasa tulizoletewa tutazitumia kulima eneo kubwa kwa muda mfupi, tutatongeza mavuno na kupata hela nyingi ” alisema Daniel Ntobi Mkulima wa Mwasubuya
“Nimeupokea mradi huu kwa furaha kabisa na nina uhakika kupitia mradi huu tutalima na kupata mazao mengi hatutakuwa na njaa lakini pia mazao mengine tutauza ili tujenge nyumba nzuri, tusomeshe watoto hata kijiji chetu kitabadilika, cha msingi hapa tuutumie vizuri” alisema Monica Severine Mkulima kutoka kijiji cha Mwasubuya
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Mhandisi. Wilbert Siogopi amesema zana za kilimo zilizokabidhiwa na Kampuni ya Agricom zitawasaidia wakulima kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga na hivyo kuongeza pato la kaya zao na kukuza uchumi wa Halmashauri na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema dhamira ya Serikali ni kuufanya Mradi wa Umwagiliaji Mwasubuya kuwa wa mfano ambao watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia watakuja kujifunza, ambapo amebainisha kuwa mpunga utakaolimwa utakuwa wa aina moja,utalimwa mara mbili kwa mwaka na hautatumia mbolea za viwandani.
Ameongeza kuwa pamoja na kilimo cha mpunga, Serikali mkoani humo imekusudia kufunga kinu cha kukoboa mpunga na kupanga madaraja ya mchele na kupitia mradi huo pia kutakuwa na ufugaji wa samaki katika Bwawa la Mwasubuya ambapo vifaranga vitawekwa na ufugaji kupitia vizimba utafanyika sambamba na kufuga samaki katika baadhi ya mashamba ya mpunga.
“Kwenye bwawa mle tutaweka vifaranga vya sangara, kambare na sato pia katika ekari zitakazolimwa ekari 10 zitatengwa ambazo mkulima atalima mpunga na kufuga samaki kwa wakati mmoja, wakati akivuna mpunga anavuna na samaki; tunataka kufunga kinu cha kukoboa mpunga na kupanga madaraja, nawaambia maisha yenu yatabadilika, hapa ni mahali tunataka kuiambia dunia Simiyu ni nini” alisema Mtaka.
Akizungumzia namna wakulima watakavyolipa deni la mkopo wa zana bora za kilimo kutoka Agricom, Mtaka amesema Halmashauri italima shamba lote ekari 514, itatoa mbegu kwa wakulima, itapanda na kuvuna na baadaye itachukua sehemu ya mavuno(gunia 10 kwa ekari) kutoka katika matarajio ya mavuno ya kati ya gunia 30 hadi 42 kwa ekari, ili kufidia gharama za uzalishaji na kurejesha deni.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Agricom, Bi Angelina Ngalula amesema kampuni hiyo inafanya kazi na Halmashauri na wakulima walio tayari na kubainisha kuwa imekopesha Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi mashine za kulimia, kupandia na kuvunia zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200 ambazo kwa mujibu wa makubaliano zitalipwa baada ya mavuno.
Mradi wa Umwagiliaji wa Mwasubuya una eneo lenye ukubwa wa ekari 700 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji na umesajiliwa kwa Jina la Umoja wa Umwagiliaji Mwasubuya (UMWASU) wenye wanachama 198.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/09/wananchi-mwasubuya-simiyu-kubabili.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa