Wananchi wa Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya hiyo Festo Kiswaga wamejitokeza kwa wingi kuchangia nguvu kazi , kuchimba msingi wa ujenzi wa madarasa zaidi 40 na mabweni 15 ya Shule ya Sekondari Simiyu
Wananchi hao wamejitokeza leo kwa wingi katika shule ya sekondari ya Simiyu kwa lengo la kuunga mkono jitihada za Mkuu wa Mkoa wao Mhe.Anthony Mtaka za kuhakikisha wanakuza na kurudisha heshima ya elimu Mkoani humo.
Wamesema kuwa wameguswa na uamuzi wa Serikali wa kuona umuhimu wa kuboresha mazingira rafiki ya kujifunzia wanafunzi na kujenga shule kubwa ya vipaji maalum ambayo itakuwa ni msaada na utambulisho wa Mkoa wao.
Yohana Musa mkazi wa mji wa Bariadi amesema kuwa wamegusa sana na uamuzi wa Serikali ya Mkoa ikiongozwa na Mkuu wao wa Mkoa Anthony Mtaka wa kuwekeza katika elimu ambayo itawasaidia watoto wao kufikia malengo waliyojiwekea.
“chini ya uongozi wa mkuu wa Mkoa pamoja na Mkuu wa Wilaya,Mkoa wetu utakuwa na shule bora itakayochukua idadi kubwa ya wanafunzi walio na vipaji maalum ndani na nje ya Mkoa wa Simiyu…Alisema Musa.
Mwenyekiti wa mtaa wa mnara wa voda Songera Magenda amesema kuwa wananchi wake wamekuwa na muamko wa kushiriki katika shughuli za kimaendeleo ili kujenga Mkoa wao.
Magenda amesema kuwa kupitia nguvu kazi za wananchi wake ,ni matumaini yake kuwa ujenzi wa shule hiyo utaenda kwa kasi na kukamilika mapema mwaka huu ambapo ukikamilika utatoa fursa kwa wanafunzi wenye vipaji maalum wa Mkoa wa Simiyu kusoma hapo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga amesema endapo shule hiyo ikikamilika itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 1000 kwani inatarajiwa kuwa na mabweni 10 pamoja na vyumba vya madarasa visivyopungua 40.
Kiswaga amesema kuwa shule hiyo imeanza kujenga kwa jitihata za uongozi wa Mkoa ambao lengo kuu ni kuona Mkoa wa Simiyu nao unakuwa na shule kubwa,nzuri ya wanafunzi wa vipaji maalum kama ilivyo mikoa mingine.
Kiswaga pia ametoa wito kwa wanasimiyu wote wenye mapenzi mema na elimu ,waone umuhimu wa kujitolea na kuchangia ujenzi wa shule hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati na kusaidia kundi kubwa na wanafunzi kusoma shuleni hapo.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA HAPA:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/04/wananchi-mkoani-simiyu-wajitokeza.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa