Wananchi takribani 1000 wa Kata ya Malambo wilayani Bariadi wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe.Festo Kiswaga wamejitokeza kuchimba msingi wa mabweni ya Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Mkoa wa Simiyu ambayo inayotarajiwa kuanza kujengwa mwezi huu .
Wakizungumza katika nyakati tofauti baadhi ya wananachi walioshiriki katika zoezi hilo wamempongeza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka kwa maono yake katika kuleta maendeleo ya elimu mkoani humo na kuahidi kuwa watahakikisha wanamuunga mkono ili malengo ya kuwa na shule ya vipaji maalum yanatimia.
“Tunamshukuru Mkuu wetu wa Mkoa kwa kuja na maono haya ya kuwa na shule ya Ufundi ya Mkoa na sisi kama wananchi wa eneo hili tunamuunga mkono kiongozi wetu, nitoe wito kwa wananchi wenzangu kila mmoja aweze kuchangia alicho na uwezo nacho ili tuweze kujenga shule yetu hii ikamilike na watoto wetu waanze kusoma” alisema Christina Matulanya Mkazi Malambo Bariadi.
Diwani wa Kata ya Malambo Mhe.Kitebo Kitebo amesema wananchi wa Kata ya Malambo kwa pamoja wameonesha ushirikiano toka walipotangaziwa kwa mara ya kwanza juu ya kuanza kwa ujenzi wa shule hiyo, hivyo akawaomba kuendelea kushirikiana mpaka shule hiyo ikamilike.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga amewashukuru wananchi wake na akawaomba waendelee kuonesha ushirikiano katika kufanikisha ujenzi wa shule hiyo ili wawe mfano bora kwa wilaya nyingine zitakapoanza kujenga shule za vipaji maalumu pia.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Bariadi Nicholaus Kasendamila amesema Jitihada hizo za Ujenzi wa Shule hiyo ya Mkoa zilizoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu lazima ziungwe Mkono ambapo amewataka Wananchi kuweka pembeni siasa kwenye suala hilo la Maendeleo
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka ambaye aliwatembelea Wananchi hao amesema Kuwepo kwa Shule hiyo ya Ufundi kutaleta chachu kubwa katika kuwapata watalaam wa fani mbalimbali katika utekelezaji wa azma ya Serikali ya awamu ya Tano ya Tanzania ya Viwanda na akawataka wazazi kuwasisitiza watoto wao kusoma kwa bidii.
“Mkoa wa Simiyu unajipambanua kama Mkoa wa viwanda ni lazima tuwe na shule ambazo watoto wetu kwenye mitaala yao wanapomaliza kidato cha nne wanakuwa na stadi za ufundi za kujiendeleza kimaisha, tunataka tujenge shule yenye karakana nzuri za ufundi watoto watakaopita hapa waweze kuendesha maisha yao, tunataka shule hii ijibu mahitaji ya mkoa” alisema
Aidha, Mtaka amesema hadi sasa wadau mbalimbali wamejitokeza kuchangia shule hiyo na mpaka sasa jumla ya shilingi milioni 157 zimetolewa na wadau hao ili kuunga mkono ujenzi wa shule hiyo na Serikali imetenga jumla shilingi milioni 58 kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Utawala.
Ameongeza kuwa baada ya kukamilisha shule hiyo ya Ufundi, Mkoa huo unatarajia kujenga shule ya Wasichana , Shule ya Wavulana na shule maalumu ya mchepuo wa Kilimo ambayo itatumika kama sehemu ya mazoezi kwa vitendo kwa Chuo cha Kilimo Sokoine(SUA).
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU TUKIO HILI FUNGUA KIUNGANISHI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/05/wananchi-wajitokeza-kuchimba-msingi-wa.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa