Wanafunzi wa shule ya sekondari Bariadi mkoani Simiyu wameomba viongozi wa mkoa na wadau wote wa elimu kuwa kambi za kitaaluma ziwe endelevu kwa kuwa zina matokeo chanya kwa katika ufaulu wa wanafunzi na ili mkoa uendelee kufanya vizuri katika mitihani yote ya Kitaifa.
Ombi hilo limetolewa tarehe 14 Aprili 2021 wakati wanafunzi hao walipopokea msaada wa chakula, shajala na taulo za kike kutoka Benki ya TPB vyote vikiwa na thamani ya shilingi 4,550,000/= ambavyo vimetolewa kwa jili ya wanafunzi wa kambi za kitaaluma kwa kidato cha sita mkoani hapa.
“Tunaomba kambi hizi ziwe endelevu maana zina mchango chanya kwenye ufaulu wa masomo yetu, miaka ya nyuma tulikuwa tukishika nafasi za mwisho kabisa lakini sasa hivi tumekuwa wa tatu Kitaifa; pia tuwaahidi tu kwamba kidato cha sita mwaka huu hatutawaangusa tutashika nafasi ya kwanza,” alisema Godfrey Andrew mwanafunzi wa kidato cha sita.
“Tunashukuru kwa msaada huu wa vitu tulivyopewa lakini pia tunashukuru kwa jitihada za mkoa kuanzisha kambi ambazo zimetusaidia kuongeza ufaulu wetu, pamoja na ufaulu kambi hizi zimesaidia wanafunzi wengi kumaliza masomo yao pasipo kukatishwa na sababu za kijamii kwani muda mwingi wanakuwa shuleni,” Minza Kija mwanafunzi wa kidato cha nne
Awali akitoa taarifa ya elimu ya mkoa Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl. Ernest Hinju amesema mkoa una mkakati wa taaluma wenye vipengele 12 na kimojawapo kikiwa kambi za kitaaluma ambazo zimechangia kuuweka mkoa katika mikoa kumi bora katika mitihani yote ya Kitaifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mikopo wa Benki ya TPB, Bw. Henry Bwogi akikabidhi msaada wa chakula, shajala na taulo za kike kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPB Benki amesema benki imetoa msaada huo kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali katika elimu.
Aidha, Bwogi ametoa rai kwa wanafunzi kujisomea kwa bidii ili waweze kufanya vizuri na kufikia ndoto zao ikiwa ni njia moja wapo ya kuthamini juhudi za viongozi wa Mkoa wa Simiyu na wadau mbalimbali katika elimu.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Mkoa, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa, Bw. Ekwabi Mujungu ameishukuru Benki ya TPB kutoa msaada huo ambao umeonesha ni namna gani wadau wa elimu wanatambua kazi inayofanywa na viongozi na wananchi wa mkoa wa Simiyu katika sekta ya elimu ambapo amewahakikishia kuwa msaada huo utatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Vile vile Mujungu amewapongeza viongozi na watendaji wa idara ya elimu mkoa wa Simiyu kwa jitihada wanazofanya katika elimu ambazo zimechangia kuuweka mkoa wa Simiyu katika nafasi nzuri ya ufaulu kwa mitihani yote ya Kitaifa, huku akiwataka wanafunzi wasome kwa bidii ili waweze kufanya vizuri na kufikia lengo la mkoa la kushika nafasi ya kwanza katika mitihani yote.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2021/04/blog-post.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa