Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewataka Wakuu wa Shule mkoani humo kuongeza ubunifu ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika shule zao.
Mtaka ameyasema hayo wakati alipokuwa akifunga mafunzo ya siku mbili kwa wakuu wa shule zote za Sekondari yaliyofanyika Mjini Bariadi katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Bariadi
Amesema wakuu wa shule wanatakiwa kuwa wabunifu hususani katika mbinu mbalimbali zitakazosaidia kuwaandaa vizuri kitaaluma wanafunzi ikiwa ni pamoja na mazoezi na mitihani ya kujipima ya mara kwa mara, zitasaidia wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani ya ndani na kitaifa.
“Kiongozi lazima uwe mbunifu, Mkiwa wabunifu kwenye shule watoto watafanya vizuri,mnapaswa kubuni mbinu na mikakati mbalimbali kwenye majaribio ya darasani, mitihani ya kujipima na kubuni namna ya kuwapa motisha walimu wenu wapende kazi na kujiona ni wanafamilia katika shule mlizopo” amesema Mtaka.
Aidha, amewataka wakuu hao wa shule kujiwekea utaratibu wa kupita mara kwa mara madarasani kukagua kwa lengo la kujiridhisha, ikiwa walimu wanatimiza wajibu wao wa kuwafundisha wanafunzi kama inavyotakiwa badala ya kusubiri kuletewa taarifa.
Mkuu huyo wa Mkoa pia amewaasa wakuu hao wa shule kuwa na uongozi shirikishi ambao unajali pande zote kwa maana ya walimu, wanafunzi na wazazi ili waweze kujua kero na masuala mbalimbali yasiyowaridhisha na waweze kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa taratibu kuyapatia suluhu.
Vile vile Mtaka amesisitiza wakuu wa shule kufanya vikao na wazazi kwa kuwa wazazi wanayo nafasi kubwa ya kuchangia wanafunzi kufanya vizuri, hivyo akawataka wavitumie vikao kupata maoni ya wazazi katika masuala mbalimbali ya kuboresha maendeleo ya wanafunzi kitaaluma.
Sanjali na hilo amewataka Wakuu hao wa Shule kuzingatia sheria, kanuni , taratibu na kuchukua hatua stahiki pale inapobidi ikiwa ni pamoja na kutowaruhusu wanafunzi wajawazito au waliojifungua kuendelea na masomo.
Kwa upande wake Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl.Julius Nestory amesema katika mafunzo hayo ya siku mbili wakuu wa shule wameelimishwa juu ya sheria zote nne za Elimu, falsafa,nyaraka,kanuni mbalimbali za Elimu na sera mpya ya Elimu.
Nestory amebainisha pia kuwa wakuu wa shule hao wamepewa mafunzo ya utunzaji wa nyaraka za Serikali, udhibiti wa vitendo vya rushwa, kusimamia shule na taaluma pamoja na utunzaji wa takwimu sahihi ambapo amewataka wakuu wa shule hao kutumia sheria zilizopo katika kusimamia shule kupitia mipango thabiti itakayotoa matokeo chanya.
Naye Magebu Bugacha Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwantimba ameshukuru uongozi wa Mkoa kuona umuhimu wa kuwaandalia wakuu wa shule mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo ambayo yatawasaidia na kuwapa uzoefu katika kuendesha na kusimamia shule zao.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Maafisa Elimu wa Wilaya za Mkoa huo, Afisa Elimu wa Wilaya ya Meatu, Mwl.Estomia Makyara amesema maelekezo yote ya Mkuu wa Mkoa aliyoyatoa wakati akifunga mafunzo hayo kwa Wakuu wa shule yatatekelezwa kwa uadilifu, ili mkoa wa Simiyu uwe ni miongoni mwa mikoa mitatu bora kwa ufaulu katika mitihani ya Kitaifa.
Jumla ya Wakuu wa shule 152 kutoka katika Halmashauri zote sita za Mkoa wa Simiyu wamepata mafunzo hayo ambayo yalilenga kuwajengea uwezo katika usimamizi na uendeshaji wa shule za Sekondari.
Baadhi ya Wakuu wa Shule za Sekondari Mkoani Simiyu wakimsikiliza Mkuu wa mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani)alipozungumza nao wakati akifunga mafunzo ya siku mbili Mjini Bariadi.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa