Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. David Kafulila ,ameyasema hayo leo, wakati wa hafla ya utoaji mikopo kwa vikundi vya wajasiriamali vilivyopo katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi. Akizungumza,Mhe.Kafulila ameeleza lengo ya Serikali katika utoaji wa mikopo ya aina hiyo ni kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwapa fursa mbalimbali yakiwemo makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kwa kuwapatia mikopo ya fedha za asilimia 10 ya mapato ya ndani yanayokusanywa na halmashauri za miji.
Fedha hizo hutokana na tozo na ushuru mbalimbali ambao hukusanywa na kuwekwa pamoja hatimaye 10% yake kutolewa kama mikopo kwa makundi maalum. "Fedha hizo ni za mikopo na sio msaada, hivyo mnawajibika kuzirejesha kwa wakati ili ziweze kukopeshwa kwa vikundi vingine, vitakavyokidhi vigezo. Nawaasa mjitahidi kuhakikisha mnatekekeleza miradi mliyoianzisha kwa ufanisi na kurejesha fedha mlizokopeshwa kama sheria, kanuni, taratibu na miongozo inavyowataka". Amesema Kafulila.
Mhe. Kafulila, amepokea hundi ya mfano kutoka benki ya NMB, yenye thamani ya Tsh. 256,090,000/-, fedha ambazo zitakopeshwa kwa jumla ya vikundi 53 vyenye wanufaika 364 kwa awamu ya kwanza katika mwaka wa fedha 2021/2022. Fedha hizo zitagawanya kwa makundi maalum vikiwa na mchanganuo ufuatao, wanawake vikunndi 37 watakopeshwa kiasi cha Tsh.180,100,000/-, vijana vikundi 11 vitakopeshwa Tsh.49,420,000/- na watu wenye ulemavu vikundi 5 watakopeshwa Tsh. 26,570,000/-.
Akizungumzia changamoto wanazokabiliana nazo katika utoaji wa mikopo ya 10% , Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bariadi Mji. Bw. Adrian Jungu, amezitaja changamoto hizo kuwa, mapato ya ndani kuwa madogo ikilinganishwa na mahitaji ya makundi maalum ya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu ambao wanaotakiwa kukopeshwa, baadhi ya vikundi kukosa uaminifu katika kurejesha mikopo, baadhi ya vikundi kubadilisha matumizi ya fedha walizokopeshwa kulingana na miradi waliyoombea mikopo, badala yake kugawana fedha au kuanzisha miradi mipya ambayo hawana uzoefu nayo na hivyo kushindwa kurejesha mikopo hiyo.
Aidha Mkurugenzi huyu ameeleeza mikakati mbalimbali ambayo Halmashauri ya Bariadi Mji imejipanga kufanya ili kukabiliana na changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapatoo ili kuongeza mapato ya ndani, kuboresha mbinu za ukusanyaji mapato kwenye vyanzo vilivyopo,kuendelea kutoa elimu kwa vikundi ili viiweze kuzingatia taratibu na miongozo iliyowekwa na kufuatilia marejesho ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani wadaiwa sugu. Hadi sasa, mashauri 6 ya madai yamefunguliwa mahakamani na tayari vikundi 2 kati ya 6 vilivyoshtakiwa vimelipa na kumaliza deni walikokuwa wanadaiwa. Halmashuri ya Bariadi Mji inadai kiasi cha Tsh. 35,057,450/- kutoka kwenye vikundi 15.
Ili kuhakikisha ufanisi katika utoaji wa mikopo hiyo Mhe Kafulila amewaagiza wakurugenzi wote wa halmashauri na wakuu wote wa wilaya za Mkoa wa Simiyu kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi ili waelewe na waitumie fursa hiyo kwani kuna watu wengi ambao hawajui kuhusu fursa hizo. Aidha amewataka wakuu hao kutumia zoezi la upandaji miti kuwa kigezo kimojawapo cha kupata mkopo. Wanakikundi wanatakiwa wapande miti ama ya kivuli ama ya Matunda na kuonyesha eneo walilopanda miti hiyo kisha ndio wapewe mkopo, hii itaharakisha na kurahisiha sana Simiyu ya Kijani.
Aidha Mhe Kafulila amewataka viongozi hao kujua watu wao wanajishughulisha na nini. "Jengeni dhana pana ya uelewa juu ya shughuli mbalimbali wanazofanya wananchi wa eneo lenu.Maafisa biashara wote ni jukumu lenu kuvijua vikundi vyote vinavyohusika na Mikopo.Maafisa biashara wote ni lazima muwe walezi wa vikundi hivi".Amesisitiza Kafulila.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa