Baadhi ya Wakurugenzi wa Mifuko na Mashirika ya Serikali hapa nchini wametembelea na kukagua maeneo yanayokusudiwa kutumika katika ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kutengeneza bidhaa zinazotumika hospitalini zitokanazo na zao la pamba na kiwanda cha maji tiba(drip) mkoani SIMIYU.
Maeneo yaliyotembelewa ni kijiji cha Nyamikoma Halmashauri ya Wilaya Busega ,kijiji cha Isenga Halmashauri ya Wilaya Bariadi na Mtaa wa Katenga Halmashauri ya Mji wa Bariadi,
Akizungumza katika kikao cha majumuisho ya ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania(TIRDO), Profesa Mkumbukwa Mtambo amesema kuanzishwa kwa viwanda hivyo kutasaidia kuokao fedha takribani shilingi bilioni 19 zinazotumika kununua maji tiba na shilingi bilioni 29 kununua bidhaa za hospitali zitokanazo na pamba kwa mwaka, ambavyo vyote kwa sasa vinanunuliwa nje ya nchi.
Profesa Mtambo ameongeza kuwa pamoja na kuokoa fedha viwanda hivyo vitatoa ajira za moja kwa moja kwa Watanzania 1600 na ajira nyingine 5000 hivyo vitachangia katika kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa wananchi wa Mkoa wa Simiyu na Tanzania kwa ujumla.
Aidha, amefafanua kuwa upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa viwanda hivi vyote viwili utkaofanywa na TIRDO unatarajia kuanza wiki sita kuanzia sasa, hivyo akawaeleza viongozi wa Mkoa wa Simiyu kuwa mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo watawasilisha taarifa itakayosaidia pia kuwaandaa wakulima kuzalisha pamba itakayohitajika kwa ajili kiwanda cha bidhaa za afya zitokanazo na pamba.
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa(MSD), Laurean Rugambwa amesema jumla ya lita 1,500,000 za maji tiba(drip) hutumika hapa nchini kwa mwaka, ambayo huagizwa nje ya nchi hivyo ameuhakikishia uongozi wa Mkoa kuwa bidhaa zitakazozalishwa katika viwanda hivyo zitapata soko la uhakika kwa kuwa zitanunuliwa na Bohari hiyo kwa ajili ya matumizi ya vituo mbalimbali vya kutolea huduma za Afya hapa nchini.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF) Bernard Kaonga amesema wanaunga mkono ujenzi wa viwanda hivyo na wamekubali kuingia kwenye ubia na TIRDO pamoja na wadau wengine kama wadau wakubwa wa afya, kwa kuwa viwanda hivyo vitasaidia kupunguza gharama ya kuagiza bidhaa hizo nje ya nchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema ni vizuri Mkoa ukapata mapema taarifa ya Upembuzi yakinifu wa kiwanda cha bidhaa za Hospitali zitokanazo na pamba ili kuendana na maandalizi ya msimu wa kilimo cha pamba, ambapo amesisitiza kuwa mkoa huo umejipanga kuongeza uzalishaji kutoka kilo milioni 70 mpaka kilo milioni 130 kwa mwaka 2018.
Ameongeza kuwa viwanda hivi vitakuwa na manufaa makubwa kwa wanachi wa mkoa huo ikiwepo suala la ajira kwa watu zaidi ya 6500 wanatarajiwa kuajiriwa katika kiwanda kitakachozalisha bidhaa za hospitali zitokanazo na zao la pamba.
“Kwa watu wa Simiyu kupata mradi utakaoajiri watu 1500 moja kwa moja, ajira nyingine 5000 pamoja na ajira za kwenye (ginneries) viwanda vyetu vya kuchambua pamba tutakuwa tumefanya kitu; ni lazima tutengeneze kura mpya za Mhe.Rais mwaka 2020, maana wapiga kura wengi wa mwaka 2020 watakuwa wapya ambao hitaji lao kubwa ni ajira na katika umri wetu huu ni lazima tujibu” amesema Mtaka.
Naye Katibu Tawala Mkoa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini amesema Wakurugenzi wa Halmashauri, Madiwani, Viongozi wa Serikali za Vijiji na Mitaa na wananchi maeneo yote yaliyotembelewa wamekubali kutoa maeneo hayo kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda, hivyo ni vema maamuzi ya mahali viwanda hivyo viwili vitakapojengwa yakatolewa mapema na wawekezaji hao ili yaweze kuandaliwa hati miliki.
Wabia wakuu katika Ujenzi wa Kiwanda cha kutengeneza bidhaa za hospitali zitokanazo na pamba na kiwanda cha kutengeneza maji tiba(maji ya drip) Mkoani Simiyu ni pamoja na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF),Bohari ya Dawa(MSD),Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA),Shirika la Viwango nchini(TBS), Benki ya Maendeleo(TIB),Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi(WCF), NEMC,TEMDO na Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania(TIRDO) ambao ndiyo wasimamizi wa Miradi hiyo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Bariadi, Ndg.Melkizedeck Humbe akitoa maelezo juu ya eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda Mtaa wa Katenga wakati wa ziara ya Wakurugenzi wa Mifuko na Mashirika waliyofanya kwa lengo la kuona maeneo kinapoweza kujengwa kiwanda cha bidhaa za Hospitali zitokanazo na pamba na kiwanda cha maji tiba Mkoani Simiyu.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda, Prof.Mkumbukwa Mtambo akizungumza na Viongozi wa Mkoa wa Simiyu katika majumuisho ya Ziara iliyofanyika katika Halmashauri ya Mji Bariadi, Halmashauri ya Wilaya Bariadi na Busega iliyofanyika kwa lengo la kuona maeneo ya kujenga kiwanda cha bidhaa za Hospitali zitokanazo na pamba na kiwanda cha maji tiba mkoani Simiyu.
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa ya Taifa(MSD), Ndg Laurean Rugambwa akizungumza katika kikao cha majumuisho ya ziara ya Wakurugenzi wa Mifuko na Mashirika waliyofanya kwa lengo la kuona maeneo ya kujenga kiwanda cha bidhaa za Hospitali zitokanazo na pamba na kiwanda cha maji tiba Mkoani Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na Wakurugenzi wa Mifuko na Mashirika na katika majumuisho ya Ziara iliyofanyika katika Halmashauri ya Mji Bariadi, Halmashauri ya Wilaya Bariadi na Busega iliyofanyika kwa lengo la kuona maeneo ya kujenga kiwanda cha bidhaa za Hospitali zitokanazo na pamba na kiwanda cha maji tiba.
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini akizungumza na Wakurugenzi wa Mifuko na Mashirika na katika majumuisho ya Ziara iliyofanyika katika Halmashauri ya Mji Bariadi, Halmashauri ya Wilaya Bariadi na Busega iliyofanyika kwa lengo la kuona maeneo ya kujenga kiwanda cha bidhaa za Hospitali zitokanazo na pamba na kiwanda cha maji tiba Mkoani Simiyu.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa