Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu Jumanne Sagini amewaagiza Waganga Wakuu wa Wilaya kuwaondoa katika nafasi za usimamizi wa zahanati na vituo vya afya ,waganga wafawidhi watakaoshindwa kusimamia vituo vyao kufika vigezo vilivyowekwa katika utoaji huduma za afya kwa wananchi kupitia mpango wa malipo kwa ufanisi (RBF).
Agizo hilo amelitoa wakati wa kikao chake na Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga Wakuu wa wilaya, Timu ya Usimamizi wa Huduma za Afya Mkoa(RHMT), waganga wafawidhi wa zahanati na vituo vya afya lengo likiwa ni kujadili matokeo ya Mpango wa Malipo kwa ufanisi (RBF) kwa kipindi cha Mwezi Januari-Machi 2018 na masuala mbalimbali yahusuyo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ikiwepo Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa.
“Waganga na Wauguzi wafawidhi tumewaita hapa tunataka mabadiliko kwenye utendaji wenu, vituo vyenu wote viende kwenye Alama A, kinyume na hapo Waganga Wakuu wa Wilaya wawavue madaraka na Waganga wakuu wa Wilaya wasipofanya hivyo Wakurugenzi washughulikieni wao” alisema Sagini.
Amesema kutotekeleza majukumu yao vizuri ikiwa ni pamoja na kushindwa kusimamia suala la ujazwaji wa takwimu sahihi kwa wakati, kunasababisha Vituo vyao kutopata fedha za mpango huo (RBF) ambazo hutolewa kwa vituo vinavyofanya vizuri, ambapo vituo hivyo vikizipata zitasaidia kuboresha miundombinu ya Afya na ununuzi wa dawa na vifaa tiba.
Ameongeza kuwa Timu za Usimamizi wa Huduma za Afya Wilaya (CHMT) zinapaswa kufanya ufuatiliaji na usimamizi katika Vituo vya kutolea huduma na kuhakikisha mapungufu yote yanayojitokeza yanafanyiwa kazi ili vituo vyote vitoe huduma kwa ufanisi na kupata fedha kulingana mwongozo wa Mpango wa RBF ambazo zitasaidia kuboresha huduma kwenye vituo.
Katika hatua nyingine Sagini amewataka Waganga wakuu wa Wilaya na Waganga Wafawidhi wa Vituo vya kutolea huduma za Afya kuwasilisha taarifa za wagonjwa wanaopata huduma kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa wakati kama maelekezo yanavyowataka kufanya ili kuondoa usumbufu usio wa lazima.
Nao Wasimamizi wa Vituo baada ya maelekezo ya Katibu Tawala wa Mkoa wamekiri kuwa watabadilika na kuhakikisha vituo vyao vinafanya vizuri na kufikia alama A ili kuwawezesha kupata fedha kupitia Mpango wa Malipo kwa Ufanisi(RBF) zitakazowasaidia kuboresha huduma za afya katika vituo vyao.
“ Nimesikitishwa sana na Halmashauri yetu kukosa fedha za RBF kiasi kilichotajwa na mratibu kwa sababu ya baadhi ya watendaji kutotimiza wajibu wao, mimi ninaona haya yote yako ndani ya uwezo wetu, kuanzia sasa tunapaswa kutimiza wajibu wetu na tuhakikishe taarifa zote zinazopelekwa wilayani zinajazwa kwa usahihi na kwa wakati” alisema Godfrey Pascal kutoka Zahanati ya Nkololo
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Bw.Fabian Manoza amesema ipo haja ya kuwajengea uwezo na kutoa mafunzo ya menejimenti ya takwimu kwa wasimamizi wa vituo vya kutolea huduma za Afya, ili waweze kukusanya takwimu zinazotakiwa kwa mujibu wa mwongozo wa Mpango wa RBF hatimaye vituo vyao vipate alama nzuri na fedha zitazowasaidia kuboresha huduma.
Kwa upande wake Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoa wa Simiyu Jarlath Mushashu ameziomba Halmashauri zote Mkoani Simiyu kulipa deni ambalo Mfuko huo unazidai lililofikia shilingi milioni 78, ili kuuwezesha mfuko huo kutoa huduma za matibabu kwa wanachama na wategemezi wao kama inavyotakiwa.
Wakati huo huo Mushashu amewaomba Wakurugenzi wa Halmashauri kuwasilisha kwa wakati michango ya watumishi ya Bima ya Afya hususani watumishi wanaolipwa kwa kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/06/waganga-wafawidhi-watakaoshindwa.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa