Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu Harold Nsekela amewataka viongozi wa Umma kuangalia maslahi ya nchi katika maamuzi wanayofanya kwa kuwa kutanguliza maslahi binafsi kunasababisha mgongano wa kimaslahi unaopelekea kuiumiza nchi.
Jaji Nsekela ameyasema hayo wakati akizungumza na viongozi wa Umma katika mafunzo ya maadili na namna bora ya kujiepusha na mgongano wa maslahi kwa Viongozi wa Umma mkoani Simiyu ambayo yamefanyika Desemba 04, 2019 Mjini Bariadi.
"Viongozi wa Umma wanapaswa kuzingatia kanuni na taratibu katiia maamuzi wanayofanya , ambazo zitasaidia kusiwepo mgongano wa kimaslahi ili kutenganisha matakwa binafsi na maslahi ya Umma katika kutekeleza majukumu, wakitanguliza maslahi binafsi wanaliumiza Taifa," alisema Jaji Nsekela.
Akizungumzia suala la ahadi ya uadilifu ambayo viongozi wa Umma hukiri mara baada ya kupewa nyadhifa mbalimbali na kuapishwa, Jaji Nsekeka amesema viongozi wa Umma wasikiri ahadi hiyo kama kasuku badala yake wawe waumini wazuri wa yale wanayoyakiri ikiwa ni pamoja na kufanya kazi zao kwa uadilifu.
Aidha, Jaji Nsekela amesema Viongozi wa Umma wanapaswa kuwa wakweli na wajaze kwa uhalali Tamko la Mali na Madeni huku akiwasisitiza kuondokana na dhana kwamba matakwa ya kisheria ya kujaza tamko hilo yanalenga kuwafilisi Mali zao kwa kuwa hakuna sheria inayozuia kiongozi wa Umma kuwa na Mali isipokuwa sheria inamtaka amiliki Mali halali zilizopatikana kwa njia halali.
Katika hatua nyingine Jaji Nsekela amewatahadharisha viongozi wa Umma kuachana na tabia ya kupokea zawadi kutoka kwa wanaowahudumia kwa kuwa jambo hilo ni kichocheo kikubwa cha rushwa, maana wao wanalipwa mishahara kwa kazi wanazofanya.
Awali akifungua mafunzo kwa Viongozi wa Umma mkoani Simiyu, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema mafunzo hayo yatawasaidia na kuwakumbusha viongozi hao kutoka huduma kwa wananchi kwa uadilifu pasipo upendeleo kwa kigezo cha dini, ukabila, kujuana na kutekeleza majukumu yao kwa wakati.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Lamadi wilaya ya Busega, Mhe. Laurent Bija amesema ili viongozi wa Umma waendelee kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu ni vema taasisi na mifumo dhabiti ya usimamizi ikaimarishwa na iwe endelevu.
Naye Katibu wa Idara ya Ukuzaji Maadili kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Bw. Waziri Kipacha amesema ikitokea kiongozi wa Umma amekiuka masharti yaliyopo kwenye Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, hatua ya kwanza ni Sekretarieti ya Maadili kufanya uchunguzi wa awali.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/12/viongozi-wa-umma-watakiwa-kuepuka.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa