Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ambaye pia ni rais wa chama cha riadha nchini Anthony Mtaka amewaagiza viongozi wa riadha kanda ya ziwa kuweka mpango mkakati endelevu wa kuwatambua na kuwaandaa kikamilifu wachezaji watakaoshiriki katika mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Mhe Mtaka ametoa kauli hiyo katika kikao na viongozi wa vyama vya riadha kanda ya ziwa kilichofanyika mjini Bariadi ambapo amesema chama cha riadha kinakabiliwa na mashindano mbalimbali ikiwemo mbio za nyika za dunia zitakazofanyika nchini Denmark, mashindano ya Afrika yatakayofanyika nchini Morocco pamoja na mashindano ya relay yatakayofanyika nchini Japan hivyo ni muhimu maadalizi yakafanyika mapema ili kuwaandaa wachezaji kisaikolojia na hatimaye waweze kurejea na ushindi.
Adha Mhe Mtaka amesema chama hicho kimeandaa utaratibu mzuri wa kuwapata wachezaji wenye viwango ambapo yatafanyika majaribio nchi nzima ili kuwawezesha viongozi na makocha kubaini vipaji vipya ili wachezaji hao waweze kujumuishwa kwenye timu ya Taifa.
“ Naomba niwahakikishia hatuwezi kupata wachezaji wazuri kama tutakaa tunalalamika, nendeni mkafanye majaribio katika ngazi za mikoa yenu, chagueni wachezaji wazuri ambao tutakuwa na uhakika watarejea na ushindi”.
“ Binafsi ninawaahidi nitawapa msaada wowote mnaohitaji, sote tunafahamu kanda ya ziwa kuna wachezaji wazuri sana, kinachohitajika ni kuweka mfumo mzuri wa kuwatambua na ndio maana tumeamua safari hii tutakuwa na makocha watano kwenye kambi zetu za taifa ambazo tunatarajia kuziweka katika mikoa ya Arusha na Pwani, mimi ninaamini tukidhamiria kuleta mabadiliko katika mchezo huu tunaweza ”, alisisitiza Mtaka.
Kwa upande wao wajumbe wa kikao hicho akiwemo mwanariadha mkongwe ambaye ni mchezaji wa kwanza kushiriki katika michezo ya Olympic mwaka 1964, Mzee Thomas Daniel walimweleza rais wa chama hicho kuwa ukosefu wa viwanja vyenye ubora, kutokuwepo kozi ya makocha wa ngazi ya juu, uhaba wa vifaa pamoja na kozi maalumu kwa ajili ya makocha ni miongoni mwa changamoto zinazohitaji kupatiwa majawabu ili kuongeza hamasa katika mchezo huo.
Kikao hicho cha siku moja kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya riadha kanda ya ziwa kutoka mikoa ya Simiyu, Mwanza, Mara na Geita.
MWISHO
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa