Mkurugenzi wa shirika la reli nchini(TRC), Bw.Masanja Kadogosa amesema kuwa shirika hilo limejipanga kuhakikisha linarahisiha huduma za usafirishaji wa marobota ya pamba kwa njia ya reli lengo likiwa kuwapunguzia gharama wenye viwanda vya kuchambua pamba.
Kadogosa amesema hayo mara baada ya kutembelea viwanda vya kuchambua pamba vya Alliance kilichopo kata ya Kasoli na NGS katika wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.
Pamoja na kupunguza gharama ameongeza kuwa njia hiyo ni salama na ya uhakika hata kipindi cha mvua mzigo unafika kwa urahisi bila matatizo ya aina yoyote huku akiongeza kuwa shirika la reli litaweka miundombinu itakayowarahisishia usafirishaji huo.
"Tumejipanga kuweka miundombinu itayowasaidia mizigo yakiwemo marobota ya pamba kusafirishwa kwa urahisi bila usumbufu wowote niwaombe wafanyabiashara watumie fursa hii ya reli kufanya shughuli mbalimbali zitakazowaingizia vipato hivyo kubadilisha maisha yao," alisema Kadogosa
Katika hatua nyingine aliongeza kuwa ni vyema jamii ione umuhimu wa kujenga viwanda vya nyama ili iwe iweze kusafirishwa nyama badala ya Mifugo ambapo mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa mikoa yenye mifugo mingi nchini .
Awali akimkaribisha mkurugenzi huyo mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema kumekuwepo na changamoto kubwa inayowakabili wafanyabiashara hususan katika usafirishaji wa robota za pamba kwani wanalazimika kutumia magari jambo linalopelekea kusafirisha mizigo michache kwa gharama kubwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu, Mhe. Enock Yakobo amewasisitiza wafanyabiashara hao kuona haja ya kutumia reli kwani huduma hiyo imesogezwa karibu na itawasaidia kuepukana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya gharama za usafirishaji na potevu wa robota za pamba.
Aliongezea kuwa ni vyema ujenzi wa eneo la kuhifadhia marobota ya pamba eneo la Malampaka ukazingatiwa huku akiongeza kuwa ujio wa usafirishaji wa kupitia njia ya reli utawarahisishia na kuwapunguzia gharama wenye viwanda vya kuchambua pamba.
Ibrahimu Kadudu ni mrajisi mkoa wa Simiyu amesema kuwa makisio ya mkoa ilikuwa kuzalisha kilogramu milioni 180 na hadi kufikia septemba 22 2019, jumla ya pamba kilogramu milioni 148,836,601 zilikusanywa kwenye vyama vya ushirika ,pamba iliyosafirishwa ni kilogramu milioni 116,391,208, iliyolipiwa kati ya pamba iliyosafirishwa ni kilogramu milioni 85,166,453 , kilogramu milioni 31,106,816 zilisafirishwa bila kulipiwa huku kiasi kilogramu milioni 32,445,393 zikiwa bado kwenye maghala na kwa baadhi ya wakulima.
Kwa upande wake meneja wa kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance ambaye pia ni katibu wa wanunuzi nchini Boaz Ogolla alisema kuwa uzalishaji umeongezeka ambapo umesababisha uhitaji mkubwa wa magari ya kusafirishia marobota ya pamba huku akitolea mfano kiwanda cha ni Alliance.
“ Kiwanda hiki kinazalisha robota 400 kwa siku na zinazosafirishwa kwa siku ni robota 200 hivyo ujio wa usafirishaji kwa njia ya reli utamaliza changamoto hiyo maana behewa moja lina uwezo wa kubeba maroboto 90 tofauti na gari lina uwezo wa kubeba marobota 25,” alisema Ogola.
Sambamba na hayo ameongeza kuwa usafirishaji huo utawapunguzia gharama ambazo sio za lazima na kuwa awali changamoto ya usafirishaji iliwalazimu kulipia mizigo kwa gharama kubwa ambapo kupitia reli watasafirisha kwa gharama nafuu hivyo kutawawezesha na wao kupata faida kwenye biashara zao.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/10/trc-yaahidi-kuwarahisishia-wachambuzi.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa