Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.David Kafulila, amewataka viongozi wa Wilaya ya Itilima pamoja na kamati ya ulinzi na usalama kuongeza ufuatiliaji wa ujenzi wa madarasa ya Uviko-19 kwani Wilaya hiyo bado ipo nyuma kwa kiwango kikubwa katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Mhe.Kafulila ameyasema hayo mara baada ya kupokea taarifa ya miradi ya ujenzi wa madarasa kwa kutumia fedha za Uviko-19,wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa madarasa hayo hivi karibuni.
“Mpaka sasa mlitakiwa muwe mmefikia asilimia zaidi ya 50, lakini mpo asilimia 20, hii kasi ni ndogo sana, ongezeni kasi tokeni maofisini nendeni site mkaangalie hali ikoje kama kuna matatizo mtatue. Mkuu wa Wilaya unatakiwa kuanzisha mkakati wa kujenga usiku na mchana, tafuteni taa, kila sehemu ambapo wanajenga waambieni wajenge usiku na mchana. Waalimu na Wasimamizi, simamieni kwa umakini na haraka ili hayo majengo yajengwe kwa kiwango bora, thamani ya pesa iwepo lakini pia msiache kuchukua hatua kwa wabadhilifu..”Amesisitiza Mhe. Kafulila.
Akitoa taarifa kuhusu kuchelewa kwa miradi hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Itilima Mhe.Faiza Suleiman ameeleza kuwa sababu ya kuchelewa kwa ujenzi wa miradi hiyo imetokana na kuchelewa kupata vifaa ikiwa pamoja na vifaa kuchelewa kufika kwenye maeneo husika kutokana na changamoto ya barabara.Aidha Mhe. Faiza alieleza kuwa ujenzi wa miradi hiyo umefikia asilimia 20 na upo usawa wa msingi katika maeneo yote.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa