Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba ameliagiza shirika la viwanda vidogo nchini SIDO kuhakikisha inawawekea wakulima mazingira bora ya utekelezaji wa shughuli za kilimo ikiwemo kupanua wigo wa upatikanaji wa zana bora zitakazoongeza thamani ya mazao yao na hivyo kuwajengea uwezo wa kupata soko la uhakika ndani na nje ya nchi.
Waziri Tizeba ametoa agizo hilo katika ziara yake ya kukagua mabanda ya maonesho ya SIDO kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu na kusema kuwa kwa muda mrefu wakulima wamekuwa wakitumia teknolojia zilizopitwa na wakati zikiwemo za kusindika mazao ya kilimo pamoja na kukoboa mpunga jambo ambalo limekuwa likipunguza ubora wa bidhaa hizo.
Aidha waziri Tizeba amesisitiza kuwa njia pekee itakayosaidia kumkwamua mkulima ni kuhakikisha anajengewa uwezo na pia anawezeshwa kupata vifaa vya kisasa kwa bei nafuu hatua ambayo amesema utekelezaji wake unategemea ushirikiano na taasisi mbalimbali zikiwemo za fedha, kilimo na viwanda.
“ Ninahitaji kuona taasisi zote zinazoguswa na shughuli za kilimo zinaweka mikakati ya kumsaidia mkulima, kwa upande wenu SIDO hakikisheni wakulima hawa wanapata mashine za kisasa za kukoboa mpunga na kusindika vyakula na pia Wizara ya Viwanda biashara na uwekezaji iwasaidie masoko pia taasisi za fedha ziwasaidie kupata mikopo, alisisitiza Waziri Tizeba’’.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka amewashauri wajasiliamali wanaoshiriki katika maonesho hayo kubadilishana ujuzi ili kila mmoja aweze kupata mbinu stahiki za kuboresha biashara yake.
Mheshimiwa Mtaka amesema kuwa wiki moja ya maonesho hayo ni sawa na darasa kwa wajasiliamali ambapo wataweza kukutana na wenzao halikadhalika wapata ushauri kutoka kwa wataalamu mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha shughuli zao huku akiwasisitiza wananchi waendelee kujitokeza kushuhudia maonesho hayo zikiwa zimebaki siku tatu kabla hayajahitimishwa.
Maonesho ya Viwanda Vidogo SIDO KItaifa yenye Kauli Mbiu: “Pamoja Tujenge Viwanda Kufikia Uchumi wa Kati” yanatarajiwa kufikia kilele chake tarehe 28 Oktoba , 2018.
MWISHO
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa