Kampuni ya Simu za Mkononi ya TIGO Mkoa wa Simiyu imetoa msaada wa karatasi kwa ajili ya maandalizi ya mtihani wa Taifa wa Kidato cha nne mkoani hapa, unaotarajia kufanyika kuanzia tarehe 23 Novemba, 2020.
Akikabidhi msaada huo jana kwa niaba ya Meneja wa TIGO Mkoa wa Simiyu, msimamizi wa Duka la TIGO Bariadi Mjini Bi. Anna Kazimoto amesema msaada huo ni mwendelezo wa ushirikiano uliopo kati ya kampuni hiyo na Mkoa wa Simiyu huku akitoa rai kwa wanafunzi kusoma kwa bidii ili waweze kufikia malengo yao.
“Tumetoa msaada huu ili ninyi ndugu zetu msome msiwe na uhaba wa karatasi kwa ajili ya kuchapisha mitihani na majaribio kwa ajili ya kujiandaa na mtihani wa Taifa wa Kidato cha nne, tumetoa rimu 45 zenye thamani ya shilingi 450,000/=” alisema Bi. Anna Kazimoto.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Simiyu, Mwl. Onesmo Simime ameishukuru kampuni ya simu ya Tigo na kuahidi kutumia msaada huo kwa matumizi yaliyokusudiwa.
Nao wanafunzi wa Shule ya Sekondari Simiyu wameishukuru Tigo kwa msaada huo na kuahidi kuwa msaada huo utawasaidia kufikia malengo yao ikiwa ni pamoja na kujiandaa vema na mtihani waTaifa kwa kuwawezesha kupata karatasi kwa ajili ya kujibia majaribiao ya mara kwa mara kuelekea Mtihani wa Taifa wa kidato cha nne.
“Mitihani inahitaji maandalizi msaada huu utawasaidia sana kidato cha nne kuondokana na uhaba wa karatasi kwa ajili ya kufanya mitihani na majaribio, tunawashukuru sana Tigo na tunaamini dada zetu na kaka zetu watafanya vizuri na hiyo itakuwa ni sehemu ya shukrani kwa Tigo,” alisema Kuyala Lameck kutoka Shule ya sekondari Simiyu.
Kwa upande wake Mwalimu Kulwa Mtanzania ameishukuru Kampuni ya Simu za Mkononi ya Tigo kwa msaada huo na kutoa wito kwa kampuni hiyo kuendelea kuwa mdau muhimu wa elimu wa mkoa wa Simiyu.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2020/11/blog-post_7.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa