Shirika la Kikristo la Life Ministry limekabidhi Zahanati kwa Uongozi wa Mkoa wa Simiyu ambayo imejengwa katika Kijiji cha Itubukilo wilayani Bariadi.
Akisoma taarifa ya makabidhiano ya zahanati hiyo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, Mkurugenzi wa Life Ministry Tanzania, Bw. Dismas Shekalaghe amesema shirika hilo lilipokea zahanati hiyo kutoka kwa wananchi ambao walianza kujenga kwa nguvu zao na kuifikisha hatua ya renta, hadi kufikia hatua za ukamilishaji wa zahanati hiyo Shirika la Life Ministry limetoa kiasi cha Shilingi milioni 71.
Amesema pamoja na zahanati hiyo, shirika hilo limefanya mengi mkoani Simiyu ikiwa ni apamoja na kutoa vifaa tiba Hospitali Teule ya Mkoa vyenye thamani ya shilingi milioni 40, huduma za macho na kutoa miwani bure, kutoa baiskeli zaidi ya 20 kwa walemavu, kugawa vifaa mbalimbali kwa makundi mbalimbali wakiwemo watoto wenye ualbino, kuwezesha vikundi vya bustani zaidi ya 40 katika kilimo cha umwagiliaji kwa njia ya matone na kuchimba visima virefu 12 vyenye thamani ya shilingi milioni 300.
Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ameishukuru Life Ministry kwa msaada wa zahanati hiyo na kuwahakikishia kuwa mara tu itakapokamilika Serikali itahakikisha Zahanati hiyo inafanya kazi na itapeleka watoa huduma za afya ili wananchi waanze kupata huduma.
"Niwakikishie tu kuwa Serikali itahakikisha Zahanati hii inafanya kazi kwa kuleta wataalam na bahati nzuri Serikali imekubali kuajiri watu wa Sekta ya Afya" alisema Mtaka.
Mtaka amesema Taasisi za Dini zimekuwa zikiunga mkono kazi mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo na akaiomba Life Ministry kuendelea kusaidia katika ujenzi wa Vituo vya kutolea huduma za Afya, ili kusaidia uboreshaji wa huduma za Afya mkoani Simiyu, kwa kuwa mkoa huo una uhitaji mkubwa wa vituo vya afya.
" Mkoa wetu tuna asilimia chini ya 40 ya vituo vya Afya, Kama ni jambo ambalo litakuwa ndani ya uwezo wa Taasisi ningeomba muendelee kutusaidia kwenye sekta ya Afya; zipo juhudi za Serikali katika uimarishaji wa sekta ya Afya hususani kwenye ujenzi wa Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali lakini washirika kama Taasisi za Dini bado tunawahitaji kwa kuwa mmekuwa mkono wa pili kwenye kuunga mkono juhudi za Serikali" alisisitiza.
Akizungumza kwa niaba ya Wananchi wa Itubukilo, Diwani wa Kata ya Itubukilo Mhe. Mayanda Makenzi akiishuku Life Ministry kwa kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo ambayo amesema itawaondolea adha wananchi wake kutembea mwendo mrefu kufuata huduma za Afya.
Naye Diwani wa Viti Maalum Mhe. Juliana Lucas amesema ukamilishaji wa zahanati hiyo utawasaidia sana wananchi kupata huduma karibu hususani wanawake ambao watapata huduma za afya ya uzazi na kupata msaada wa karibu wakati wa kujifungua na hivyo kupunguza vifo vya wakina mama na watoto.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Bw. Abdallah Malela amesema Zahanati hiyo ya Itubukilo itafunguliwa rasmi na kuanza kutoa huduma Julai Mosi, 2018.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA KIUNGANISHI:- https://simiyuregion.blogspot.com/2018/06/simiyu-yakabidhiwa-zahanati-na-shirika.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa