Mkoa wa Simiyu umejipanga kuhakikisha vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga vinapungua kwa kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imewekeza na kutumia gharama kubwa katika kuandaa wataalam(wakunga) wenye jukumu la kuhakikisha wanatoa huduma zitakazotoa majibu sahihi ya utatuzi wa changamoto hiyo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga wakati akifunga mafunzo ya wakunga yanayohusu utoaji wa huduma za dharura kwa wakina mama na watoto wachanga chini ya mradi wa Mkunga Okoa Maisha, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka yaliyohusisha wakunga kutoka katika Halmashauri zote sita mkoani humo.
Kiswaga amesema pamoja na kuwepo dalili za kupungua kwa vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga mkoani huo bado ipo haja ya kujitathmini ili kubaini ukubwa wa tatizo kama njia ya kulipatia ufumbuzi wa kudumu.
“ Ni kweli ukilinganisha takwimu za mwaka jana na mwaka huu zinaonyesha idadi ya vifo vinavyotokana na matatizo mbalimbali ya uzazi vimepungua, lakini naomba niwape angalizo, tusizichukulie takwimu hizi kama kigezo cha ubora wa huduma zinazotolewa katika vituo vyetu, bali iwe chachu ya kufanya kazi kwa bidii ili fikapo mwezi Desemba mwaka huu tuwe katika nafasi ya juu zaidi”.
Aidha Kiswaga amewaasa wahitimu wa mafunzo hayo kuhakikisha wanaitumia kikamilifu elimu waliyoipata ili iwawezeshe kukabiliana na dharula wakati wa kuwahudumia wakina mama wajawazito na watoto wachanga na kuongeza kuwa serikali haitamvumilia mkunga yeyete atakayetumia kisingizio cha aina yoyote kwa kusababisha kifo cha mama au mtoto.
Halikadhalika Kiswaga ameishukuru serikali ya Canada kupitia chama cha wakunga cha nchi hiyo CAM na kusema kuwa imefanya uamuzi sahihi wa kuisaidia Tanzania katika eneo hili nyeti la kuwajengea uwezo wataalamu hao watakaotumika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto na kuahidi kuwa serikali iko tayari kupokea ushauri utakaosaidia kukabiliana na changamoto hiyo.
Kwa upande wake rais wa chama cha wakunga Tanzania TAMA Feddy Mwanga amesema tafiti za hivi karibuni zinaonyesha kuwa mkunga mwenye mafunzo yuko katika nafasi nzuri zaidi ya kukabiliana na changamoto zinazowakabili akina mama wajawazito na watoto wachanga kwa 87%.
“ Hivyo kwa sisi wakunga tunaamini hatua hiyo ni nzuri na kwamba kinachofuata sasa ni kuwahimiza wakina mama wahudhurie kliniki mapema na kwa wakati na hapa ndipo tunaweza kupima mafanikio ya mpango huu kupitia kwa wahitimu hawa tunaowakabidhi vyeti hii leo” alisema Bi Mwanga.
Akizungumza kwa niaba ya wahitimu wa mafunzo hayo yaliyobebwa na kauli mbiu ya Mkunga Okoa Maisha -Jonas Julius ameiomba Serikali kuboresha mazingira yao ya kutolea huduma ikiwemo kuwapatia nyumba za kuishi jirani na vituo vya kazi sambamba na kuwaendeleza kitaaluma ili waweze kukabiliana na changamoto zinazojitokeza.
Mkoa wa Simiyu una jumla ya wakunga 500 ambapo kupitia mpango huo jumla ya wakunga 220 wamenufaika na mafunzo hayo yanayofadhiliwa na CUSO International, Chama cha wakunga Tanzania (TAMA) pamoja na Chama cha wakunga Canada (CAM) .
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/09/serikali-mkoani-simiyu-yajipanga-kuzuia.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa