Uongozi wa Mkoa wa Simiyu umefunga kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi wa kidato cha Sita mwaka 2020 iliyokuwa ikifanyika katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa , ikiwa ni sehemu ya tahadhari dhidi ya Homa kali ya Mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona.
Akifunga kambi hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amesema uongozi wa mkoa umefikia hatua hiyo kuchukua tahadhari kama ilivyoelekezwa na viongozi mbalimbali wa Kitaifa juu ya kuzuia mikusanyiko ya watu wengi isiyo ya lazima katika kipindi hiki ambacho kumeripotiwa idadi ya watu kadhaa kubainika kuwa na virusi vya Corona katika nchi mbalimbali.
“Kutokana na Maelekezo ya Serikali Mkoa umeona kambi hii ifungwe kwa ajili ya tahadhari dhidi ya Corona, Mhe. Rais amesitisha mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2020, Mhe. Waziri Jafo amesitisha UMISETA na UMITASHUMTA na tahadhari mbalimbali zimeendelea kutolewa na Serikali ikiwemo ya kuzuia mikusanyiko; sisi hapa tuna wanafunzi takribani 1000 kutoka shule 10 hivyo tumekubaliana kwa pamoja tuifunge kambi hii,” alisema Sagini.
Aidha, Sagini amesema pamoja na kambi za kitaaluma kufungwa Mkoa utaendelea kusimamia utekelezaji wa mkakati wa taaluma wa mkoa ili walimu, wanafunzi na wadau wengine wa elimu waweze kutimiza wajibu wao kuhakikisha Mkoa unatimiza adhma yake ya kuwa miongoni mwa mikoa itakayofanya vizuri katika mitihani yote ya Kitaifa.
Kwa upande wake Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl. Ernest Hinju amesema wanafunzi hao walitakiwa kukaa kambini muda wa wiki sita kwa ajili ya maandalizi ya Mtihani wa Taifa unaotarajiwa kufanyika mwezi Mei 2020, hivyo pamoja na kusitisha kambi hiyo walimu wamehimizwa kutimiza wajibu wao katika ufundishaji na wanafunzi wametakiwa kwenda kusoma kwa bidii ili kufikia lengo la Mkoa.
Awali akitoa elimu ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona kwa wanafunzi na walimu kabla ya kambi kufungwa, Afisa Afya wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Reuben Malimi amesema ugonjwa huo hauna tiba matibabu yanayofanyika yanazingatia dalili zinazoonekana kwa mgonjwa, hivyo ni vema kila mmoja akachukua tahadhari kwa kuzingatia maelekezo na elimu inayotolewa na wataalamu wa afya katika maeneo mbalimbali.
Nao wanafunzi wa Kidato cha Sita wa Mkoa wa Simiyu wameshukuru uongozi wa Mkoa kuchukua tahadhari dhidi ya Virusi vya Corona kwa kutoa elimu kuhusu Corona kabla ya kufunga kambi, huku wakieleza namna ambavyo kufungwa kwa kambi kunaweza kuathiri malengo yao waliyojiwekea.
“Tunashukuru uongozi wa Mkoa kutoa elimu na kuchukua tahadhari ya Corona kwa kufunga kambi ni hatua ya kutuhakikishia usalama, lakini kambi ilitusaidia kujua namna ya kujibu maswali ya mtihani wa Taifa na kujifunza mada ngumu tulizoshindwa shuleni kupitia kwa walimu mahiri, tutatumia muda huu kujisomea kwa bidii ili tufaulu vizuri mtihani wa Taifa,” alisema Isack Ndassa kutoka Shule ya Sekondari Kanadi Itilima.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2020/03/simiyu-yafunga-kambi-ya-kitaaluma.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa