Bariadi.
Mkoa wa Simiyu umepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa malengo matatu ya kimataifa ya 95:95:95 katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI ambayo ni kuhakikisha Wananchi wenye maambukizi ya VVU wanatambua hali zao,utoaji wa dawa za kufubaza makali ya VVU kwa waliobainika kuwa na maambukizi, pamoja na utoaji hamasa kwa waliobainika kuwa na maambukizi kutumia Dawa.
Hayo yamebainishwa na kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu Wakili Mwanahamisi Kawega alipofungua mkutano wa Tathmini ya robo ya kwanza ya mwaka wa mradi wa Afya Thabiti, wenye lengo la kupokea taarifa ya utendaji kwa kipindi cha robo ya kwanza (October-December 2023) uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Bariadi Comference lengo likiwa ni kujadili mafanikio, changamoto na mafunzo yaliyopatikana wakati wa utekelezaji wa mradi wa Afya Thabiti wenye lengo la kutoa huduma za VVU/UKIMWI katika mikoa ya Simiyu na Mara.
“Lengo la kwanza la kuhakikisha wananchi wenye maambukizi ya VVU wanatambua hali zao limefikiwa kwa asilimia 100.4%, ikilinganishwa na lengo la asilimia 95%. Lengo la pili la kuwapa dawa wenye VVU limefikiwa kwa asilimia 96.7%, na lengo la tatu la kuwahimiza watu hao kutumia dawa ili kufubaza virusi vya UKIMWI limefikiwa kwa asilimia 97.4%, ikilinganishwa na lengo la asilimia 95%.” Alisema Wakili Kawega.
Aidha Wakili Kawega amewapongeza Wataalamu wa Afya Mkoani Simiyu kwa mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa malengo matatu ya kimataifa ya 95:95:95 katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI ambapo amewataka kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kundi la Vijana kuanzia miaka 0-24 linafikiwa na kupatiwa hamasa ya kutosha ili waweze kujitambua na kupima Afya zao kusudi wale watakaobainika waweze kuanza matumizi ya Dawa za kufubaza makali ya VVU.
Ernest Kisandu, Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) amesema Wizara itaendelea kutoa ushirkiano kwa Wadau mbalimbali wa kupambana na VVU na UKIMWI Nchini kusudi malengo mahsusi ya kutokomeza VVU yaweze kutimia.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt.Boniface Marwa amesema Pamoja na mafanikio hayo ipo changamoto kwa kundi la Vijana wenye umri wa kuanzia 0 hadi 24 ambalo bado halijafikia viwango vya kutambua hali zao za VVU na kutumia dawa ambapo mkoa unajipanga kwa kushirikiana na wadau kuhakikisha kuwa kundi hilo linafikiwa.
.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa