Mkoa wa Simiyu unatarajia kufanya majaribio ya kufundisha wanafunzi kwa kutumia mtandao kupitia programu itakayotengenezwa na watalaam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka katika Maadhimisho ya Wiki ya Elimu Mkoani humo yaliyofanyika kimkoa mjini Mwanhuzi Wilayani Meatu, chini ya Kauli Mbiu “TUWEKEZE KATIKA ELIMU KWA USTAWI WA JAMII YENYE UTAALAMU WA SAYANSI NA VIWANDA KUELEKEA UCHUMI WA KATI TANZANIA”
“Tunataka tufanye majaribio, tuanze kwa kuunganisha shule zetu za mjini wataalamu wetu wa ICT (TEHAMA) watengeneze programu,baadhi ya madarasa kama darasa la saba tuanze kufundisha kwa kutumia mtandao” amesema.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wanafunzi walioshiriki katika maadhimisho ya wiki ya elimu wamesema iwapo teknolojia hiyo itafanikiwa kutumika itawasaidia katika masomo yenye upungufu wa walimu hususani wa sayansi, ambapo wameiomba Serikali kuendelea kutatua changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa na vifaa vya maabara ili kuwawezesha kujifunza vema masomo hayo kwa nadharia na vitendo.
Kwa upande wake Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Julius Nestory amesema maadhimisho ya wiki ya Elimu yaliyoanza Mei 24 ni moja ya tathmini ya malengo yaliyowekwa Mei 2016 na miongoni mwa mafanikio ya malengo hayo ni ujenzi wa vyumba vya madarasa zaidi ya 180 chakula cha mchana kutolewa katika shule za kutwa lililotekelewa kwa asilimia 43.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe Anthony Mtaka amesema Serikali imepanga kupitia Watalaam hao wa TEHAMA pia kwa kutumia teknolojia nyepesi, itengenezwe programu itakayosaidia kutoa taarifa za uwepo wa watumishi mahala pa kazi.
Aidha ameongeza kuwa katika kipindi hiki ambacho Serikali Mkoani Simiyu imejipanga kufanya mapinduzi ya Viwanda, imedhamiria kuwatumia Watalaam wa TEHAMA kutengeneza mfumo wa taarifa na takwimu sahihi za kila sekta zikiwemo za kilimo, mifugo, elimu ili mtu akitaka taarifa yoyote ya Simiyu azipate kwa urahisi (awe nazo mkononi).
“Miaka minne ijayo hatutakuwa na Simiyu mnayoiona leo, kama kuna mtu anafikiri ni maneno atupe muda; tunataka tuwapunguzie Watanzania kufanya rejea nchi nyingine waje kwenye mkoa wetu. Tarehe 09/05/2017 Maswa wanapokea hundi ya shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha chaki Maswa, Meatu upembuzi yakinifu unaanza tarehe 12/06/2017 ujenzi wa kiwanda cha maziwa” amesema.
Wakati huo huo Mkuu huyo wa Mkoa amesema Serikali inalitafutia ufumbuzi wa kudumu suala la bei ya pamba ambalo limekuwa likiwakatisha tamaa wakulima kwa kuwa wafanyabiashara wananunua pamba kwa bei ya chini kwa kigezo cha kuwa bei katika soko la dunia iko chini.
Mtaka amesema Simiyu inaoongoza kwa kulima pamba lakini Halmashauri na wananchi hawanufaiki kwa kiwango kinacholingana na uzalishaji uliopo, hivyo watatafutwa watalaam ambao watachunguza bei ya pamba katika soko la dunia na akasisitiza kuwa mfanyabiashara yeyote atakayeona pamba haina faida kwake aache katika Msimu wa mwaka 2018 Halmashauri zitanunua.
Wiki ya Elimu huadhimishwa kila mwaka mwezi Mei ikiwa na lengo la kuwakutanisha wadau wa elimu, kuona shughuli mbalimali za elimu, kufanya tathmini ya mipango ya elimu ya mwaka uliopita na kuweka mipango ya mwaka mwingine.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa