Mkoa wa Simiyu umejipanga kuanza kuwaandaa Wanafunzi wa Darasa la Saba na Kidato cha Nne wa mwaka 2019 kuanzia mwezi Agosti, mwaka huu 2018 ili kufikia malengo ya kuongeza ufaulu katika mitihani yote ya Taifa.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Anthony Mtaka katika Hafla fupi ya kuwapongeza walimu wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi kwa kuongeza ufaulu kwa Shule za Msingi na Sekondari kipindi cha miaka miwili mfululizo, iliyofanyika Ukumbi wa Bariadi Alliance Mjini hapa.
Mtaka amesema kutakuwa na mitihani kwa wanafunzi wa darasa la sita na kidato cha tatu mwezi Agosti 2018 ili kupata wanafunzi wenye ufaulu mzuri watakaounda darasa maalumu la darasa la saba na kidato cha nne mwaka 2019 ( special class).
"Tunaanza maandalizi ya darasa la saba na kidato cha nne wa mwakani kuanzia mwezi Agosti mwaka huu, ili tuchuje bila kupendelea mtihani ni chujio zuri, matokeo hayo yatabandikwa na wazazi wote wataona" alisema Mtaka.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema baada ya kumaliza kambi ya kitaaluma kwa kidato cha sita mwezi huu, Mkoa umepanga kufanya kambi za kitaaluma kwa kidato cha nne na darasa la saba ambazo zitafunguliwa rasmi tarehe 06 Juni, 2018.
Wakati huo huo amesema Serikali inaendelea kuwajengea uwezo walimu mahiri na makini ili waweze kuwasaidia wanafunzi wa madarasa maalumu kufanya vizuri lengo likiwa ni kuongeza ufaulu kwa shule za msingi na kufuta daraja la nne na sifuri kwa shule za sekondari.
Kuhusu ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mkoa, Mtaka amesema Mkoa utajenga shule ya Mkoa Mjini Bariadi (Makao Makuu ya mkoa) ambayo itatambulika kama Shule ya Sekondari Simiyu na itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1000 huku ikiwa na miundombinu mingine muhimu kama maabara, vyumba vya kompyuta na mkongo wa Taifa.
Pia amesema pamoja na kujenga Shule hiyo ya Mkoa, Serikali imedhamiria kwa kushirikiana na wananchi kujenga shule mbili maalumu kwa ajili ya wasichana na wavulana (Simiyu Girls na Simiyu Boy's) ambazo zitabeba taswira ya Mkoa na kutambulisha Mkoa huo tofauti na ilivyo sasa ambapo shule nyingi zilizopo katika Makao makuu ya Mkoa ni zile za Kata.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewaruhusu walimu mkoani humo kufundisha masomo ya ziada (tuition) hususani wakati wa likizo na mapumziko ili wanafunzi waendelee kujifunza badala ya kusubiri kufundishwa darasani pekee.
Akizungumza kwa niaba ya walimu wa Halmashauri ya Mji, Mwl. Travel Ndimangwa kutoka Shule ya Msingi Somanda A amepongeza utaratibu wa kuwaandaa wanafunzi wa madarasa ya mitihani pamoja na kuruhusiwa kuwafundisha wanafunzi masomo ya ziada mambo ambayo amesema yatachangia kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Mhe. Robert Lweyo ametoa wito kwa walimu wa Halmashauri hiyo kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kupandisha ufaulu ambapo mwaka 2017 ilishika nafasi ya 22 Kitaifa katika mtihani wa Kidato cha Nne kutoka nafasi ya 44 mwaka 2016
PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA HAPA:-.https://simiyuregion.blogspot.com/2018/04/simiyu-kuanza-kuwaandaa-wanafunzi-wa_24.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa