Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe. Festo Kiswaga amesema Serikali mkoani Simiyu itaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na watu wenye ulemavu wa makundi yote bila kubagua na kuhakikisha wanapata huduma kwa wakati katika taasisi za Serikali wanapoenda kupata huduma.
Kiswaga ameyasema hayo Juni 13, 2019 wakati wa alipofungua kikao cha uboreshaji huduma kwa jamii ya viziwi Mkoa wa Simiyu, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, kilichofanyika Mjini Bariadi.
Amesema watu wenye ulemavu wana haki sawa na watu wengine hivyo akatoa wito kwa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na maeneo mengine ya kutoa huduma za jamii mkoani Simiyu kufanya utaratibu wa kuweka wataalam maalum wenye uelewa wa lugha ya alama ili kuondoa changamoto ya mawasiliano kwa watu wenye ulemavu hususani viziwi.
“Vyombo vya ulinzi na usalama vihakikishe vina mtu au watu kwa ajili ya kuwasaidia viziwi kuondoa changamoto ya mawasiliano pamoja na watu wenye ulemavu kwa ujumla wanaohitaji huduma, si lazima kuajiri kwa sasa kwa kuwa suala la ajira linaweza kuchukua muda; lakini wahakikishe wana mtu wa kutoa msaada viziwi wapate huduma” alisema Kiswaga.
Aidha, Kiswaga amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa viziwi kuhusu maeneo yaliyozuiwa kama vile katika vyombo vya ulinzi (majeshi) na kushauri kuwa ikiwa wanapaswa kwenda katika maeneo hayo waombe msaada kwa watu wenye uwezo wa kuzungumza ili kuepuka watu hao kuonekana kuwa wamevunja sheria kwa kukusudia kwenda maeneo hayo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Tanzania(CHAVITA) Mkoa wa Simiyu, Mhandi Zephania amesema viziwi wanakabiliwa na changamoto ya mawasiliano wanapoenda kupata huduma mbalimbali hivyo chama hicho kinaendelea kutoa elimu ya lugha ya alama kwa watumishi wa maeneo mbalimbali ya kutolea huduma ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Naye Mkalimani wa lugha ya alama Bw. Jonathan Livingstone amesema Wizara ya Elimu imekubali kupokea jukumu la kusanifisha lugha ya alama iingizwe katika mitaala ifundishwe katika shule za msingi, sekondari na vyuo.
Katika hatua nyingine Kamanda wa Wilaya ya Maswa, Jonas Nyaoga amesema Jeshi la polisi limejipanga kuwahudumia viziwi kwa namna ambayo wakiwa wanahitaji huduma wanasaidiwa kwa kuhakikisha kuwa kila wanapowahoji viziwi wanatafuta watu wanaofahamu lugha ya alama ili waweze kuwatafsiria.
Kikao cha kujadili uboreshaji wa huduma za jamii kwa viziwi mkoani Simiyu kilijumuisha viongozi wa Chama cha Viziwi(CHAVITA) Mkoa wa Simiyu, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya zote tano za Mkoa wa Simiyu.
MWISHO
KUPATA HABARI KAMILI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/06/serikali-mkoani-simiyu-itaendelea.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa