Shirika la Mendeleo la Uingereza (DFID) kupitia Mpango wa Kuboresha Elimu Tanzania(EQUIP-T) limetoa jumla ya shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya ujenzi wa Miundombinu ya Elimu katika Halmashauri zote za mkoa wa Simiyu.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka wakati wa hafla fupi ya makabidhiano na vyerehani 50 kutoka Ubalozi wa China, kusaini hati ya makubaliano ya ujenzi wa Bweni la Wasichana Shule ya Sekondari Nkoma Itilima, Makabidhiano ya. Hundi ya Shilingi Milioni 178 kwa ajili ya ujenzi wa bweni hilo zilizotolewa na Balozi wa China, na uwasilishwaji wa Taarifa za mashirika wadau wa Maendeleo mkoani Simiyu(DFID, AMREF na UNFPA), ambayo ilishuhudiwa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan.
Mtaka amesema fedha hizo zimeshapokelewa katika Akaunti za Halmashauri zote za Mkoa huo na wiki ya kuanzia tarehe 26/02/2018 Halmashauri hizo zinaanza kujenga miundombinu ya Elimu.
Mtaka ametoa shukrani zake kwa Shirika hilo ambalo amesema limechangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko katika Elimu na kuufanya mkoa wa Simiyu kutoka kwenye nafasi za mwisho kwenye ufaulu mpaka kufikia nafasi ya 11 kwa mwaka 2017.
“ Tunawashukuru sana DFID kwa namna wanavyotusaidia katika Sekta ya Elimu kwenye mkoa wetu, DFID kupitia EQUIP wametoa IPAD(Vishikwambi) kwa kila Mkuu wa Shule ndani ya mkoa Simiyu, Kila Mratibu wa Elimu wa Elimu Kata amepewa pikipiki na anapewa posho ya shilingi 206,000/= kila mwezi kwa ajili ya kununua mafuta ya kuwawezesha kutembelea shule zao, sisi kama mkoa tunawashukuru sana” alisema Mtaka.
Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID) Bi. Elizabeth Arthy amesema Shirika hilo litaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali na kuhakikisha wanashiriki katika kuinua ubora wa elimu kwa watoto wa Mkoa wa Simiyu.
Naye Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke aliyekabidhi vyerehani 50 kwa ajili ya Kikundi cha Wanawake Mjini Bariadi amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka kwa jinsi anavyojishughulisha katika kuwaletea wananchi wa Mkoa wa Simiyu maendeleo na akaahidi kuendelea kushirikiana na mkoa huo katika nyanja mbalimbali.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika lilaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani(UNFPA), Bi. Jacqueline Mahon amewapongeza viongozi wa mkoa wa Simiyu wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka na akaahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo mkoani humo kupitia huduma za afya ya uzazi kwa wananwake na vijana.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Simiyu, Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mhe.Andrew Chenge, aliyashukuru mashirika hayo na Balozi wa China ambao ni wadau wakubwa wa maendeleo mkoani humo katika Sekta ya elimu, afya na viwanda na kubainisha kuwa mkoa huo una kiu ya maendeleo ni hivyo umejipanga kwenda kwa kukimbia wakati wengine wanatembea.
MWISHO
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa