Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewahakikishia wafanyabiashara mkoani hapa kuwa Serikali itatatua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji na umeme kupitia mradi wa maji wa ziwa Victoria, uimarishwaji wa mamlaka za maji na kujengwa kwa vituo vya kupozea umeme.
Mtaka ameyasema hayo wakati ufunguzi wa hoteli ya Sweet Dreams iliyoko Mjini Bariadi na kumpongeza mfanyabiashara John Sabu kwa uwekezaji huo.
Amesema Mkoa unaendelea kuimarisha vyanzo vya maji na mamlaka za maji na kufikia mwaka 2020 maji kutoka Ziwa Victoria yatakuwa yameshafika katika makao makuu ya mkoa, huku akibainisha kuwa tatizo la umeme litatatuliwa na ujenzi wa vituo vya kupozea umeme.
“Sisi tuna mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Victoria ambao (kwa maelezo ya Waziri wa Maji) mpaka mwezi Februari 2019 watakuwa wametangaza zabuni ya ujenzi wa mradi huo ili maji yafike hapa, kwa kuanza mpaka kufikia mwaka 2020 maji yatakuwa yamefika makao makuu ya mkoa”
“Kwenye umeme tumezungumza na watu wa Wizara ya Nishati, tutajengewa (sub-stations) vituo viwili vya kupozea umeme, kwa kuanzia kimoja kitajengwa mwaka huu kwa hiyo tutakuwa na umeme wa uhakika” alisisitiza Mtaka.
Katika hatua nyingine Mtaka amewataka Wakuu wa Wilaya kuwalinda wafanyabiashara wakubwa na wadogo na kuwasaidia kutafsiri sheria, miongozo na taratibu zinazopaswa kuwasaidia kufanya biashara zao katika mazingira mazuri, huku akisisitiza biashara ziendelee kufanyika saa 24.
Kwa upande wao Wafanyabiashara wamempongeza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka kwa kuwaruhusu kufanya biashara saa 24 na wakamuahidi kuwa wataendelea kuwekeza katika ujenzi wa vitega uchumi mbalimbali ikiwemo hoteli za kisasa na kuendelea kuwa walipa kodi waaminifu.
“Tunamshukuru Mhe. Mkuu wa mkoa kwa kuruhusu wafanyabishara tufanye biashara zetu saa 24 tunamuahidi kuwa tutaendelea kufungua biashara mbalimbali kama hoteli ili kuondoa adha ya malazi kwa wageni wanaofika hapa mkoani, pia tutaendelea kuwa walipa kodi halali wa nchi yetu” Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mhe. Njalu Silanga.
Awali akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa Hoteli ya Sweet Dreams mtoto wa Mmiliki wa hoteli hiyo, Mary John Sabu amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka kwa ubunifu na ushawishi wake uliopelekea matukio mengi ya Kitaifa kufanyika mkoani Simiyu, ambayo yamechangia kuongeza mzunguko wa biashara mkoani hapa.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/01/serikali-yawahakikishia-wafanyabiashara.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa