Rais Mstaafu wa Awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Benjamin William Mkapa amesema Serikali imeondoa zuio la kuuza Mazao ya Chakula nje ya nchi ikiwa ni njia nyingine ya kuongeza soko la mazao ya wakulima hapa nchini.
Mhe. Mkapa amesema hayo katika Kilele cha Maonesho ya Nane nane Kitaifa mwaka 2018 Mkoani Simiyu, Uwanja wa Nyakabindi, Halmashauri ya Mji wa Bariadi ambapo alikuwa mgeni Rasmi akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
“Ninachukua fursa hii kuwafahamisha kuwa Serikali imeondoa zuio la kuuza Mazao ya Chakula nje ya nchi ikiwa ni njia nyingine ya kuongeza soko la mazao ya wakulima hapa nchini, hata hivyo mazao hayo yatauzwa nje ya nchi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu”alisema.
Aidha, amesema Serikali inawakumbusha wananchi wote kuhifadhi akiba ya kutosha ya chakula wakati wa kuuza mazao yao ili kujihakikishia usalama wa chakula katika kaya zao.
Mkapa pia amesema Serikali ina mkakati wa kuongeza uzalishaji wa zao la pamba kutoka tani 121,000 mwaka 2016/2018 hadi kufikia tani milioni moja mwaka 2020.
Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba ametangaza rasmi kuwa Maonesho ya Nane nane Kitaifa kwa miaka mitatu mfululizo hadi mwaka 2020 yatafanyika kanda mpya Kanda ya Ziwa Mashariki katika Uwanja wa Nyakabindi Bariadi, huku akisisitiza kuwa maonesho hayo yafanyike Kimataifa kwa kushirikisha nchi jirani zinazoizunguka Tanzania.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka amesema Mkoa wa Simiyu utaendelea kulipa kiupaumbele zao la Pamba na mwaka ujao uzalishaji utaongezeka kutoka kilo milioni 70 hadi kufikia kilo 150.
“Simiyu tunajivunia wananchi wachapa kazi wenye uthubutu na Simiyu inajengwa na Wanasimiyu, mwaka jana tumezalisha kilo milioni 70 za pamba, kwa mwaka huu sasa hivi msimu ukiwa umefikia katikati tuna kilo milioni 85, mwakani tunatarajia kuzalisha kilo zaidi ya 150” alisema
Ameongeza kuwa wananchi wamelima chakula cha kuwatosheleza si watu wa kuomba chakula cha msaada huku akiupambanua Mkoa wa Simiyu kuwa ni mkoa pekee ambao watu wake wanafanya biashara saa 24.
Maonesho ya Nanenane Mwaka 2018 yaliwashindanisha wakulima na wafugaji mmoja mmoja, Taasisi, Wakala, Mashirika ya Umma na Binafsi, Wizara pamoja na Halmashauri 21 za Mikoa ya Simiyu Mara na Shinyanga ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Maswa imekuwa ya tatu kati ya hizo 21.
Kauli mbiu ya Maonesho ya Nanenane mwaka 2018 “ WEKEZA KATIKA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI KWA MAENDELEO YA VIWANDA”
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:https://simiyuregion.blogspot.com/2018/08/serikali-yaondoa-zuio-la-kuuza-mazao.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa