Naibu Waziri wa kilimo, Mhe. Omary Mgumba amesema Serikali imekaa na wanunuzi wa pamba na kwa pamoja wamekubali kuanza rasmi kununua pamba kwa bei elekezi ya shilingi 1200 na ikiwa kutakuwa na hasara watakayopata kutokana na bei ya zao hilo kushuka katika soko la dunia (baada ya Agosti 15, 2019 )Serikali itafidia.
Mhe. Mgumba ameyasema hayo katika nyakati tofauti wakati akiwa kwenye ziara yake ya kukagua mwenendo wa ununuzi wa zao la pamba katika Wilaya ya Bariadi na Maswa Mkoani Simiyu.
Amesema awali wanunuzi wengi walisita kununua pamba kwa bei kubwa na kuuza kwa bei ndogo kutokana na kushuka kwa bei ya pamba katika soko la dunia, lakini Serikali kwa kuwathamini wakulima, imesema pamba itanunuliwa kwa shilingi 1200 na ikiwa kuna hasara zozote za kibiashara watakazopata wanunuzi baada ya tarehe 15/08/2019 serikali itafidia.
“Tumekubaliana na wanunuzi kuwa waingie rasmi sokoni wanunue kwa bei elekezi ya shilingi 1200 kama kuna kushuka bei au kutakuwa na hasara yoyote hayo Serikali itabeba lakini wao waendelee kununua pamba kupitia vyama vya ushirika, msikubali kuuza pamba yenu chini ya bei ya shilingi 1200” alisema Mhe. Mgumba.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bariadi mhe. Festo Kiswaga amesema tayari wanunuzi wawili ambao ni NSAGALI na NGS Company wamepeleka fedha katika Vyama vya ushirika vya Msingi wilayani Bariadi na wanunuzi wengine wanaendelea kwenda kununua.
Nao wakulima waliotembelewa na Mhe. Naibu Waziri wa Kilimo wameiomba Serikali kutoa mbegu, dawa na viuatilifu kwa wakati ili waweze kuongeza tija katika uzalishaji jambo ambalo Mhe. Mgumba alilitolea ufafanuzi kuwa linaendelea kushughulikiwa kwa kusajili wakulima ili kujua idadi kamili ya wakulima na kutoa pembejeo za kutosha kulingana na idadi ya wakulima.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa kilimo, Mhe. Omary Mgumba ametoa pole kwa wakulima wa Kijiji cha Shinyanga Mwenge wilayani Maswa kwa naiba ya Serikali kutokana na tatizo walilopata la kuunguliwa na pamba yao katika ghala ya Chama cha Ushirika cha msingi na kuelezwa kusikitishwa sana na tukio hilo.
Akitoa salamu hizo za pole kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema Serikali imesikitishwa sana janga hilo na iko pamoja nao, huku akitoa wito kwa wanachama wa Chama cha Ushirika cha Msingi kuchukua tahadhali ya moto katika maeneo waliyokusanya pamba.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Seif Shekalaghe ametoa wito kwa wanachama wa vyama vya ushirika kuchagua viongozi waadilifu.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/07/serikali-yakubaliana-na-wanunuzi.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa