Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa SIMIYU.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu Julai 12, 2018, mara baada ya kukagua ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje(OPD) la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu, ambapo ameridhishwa na ujenzi wa jengo hilo.
Waziri Ummy amewahakikishia viongozi wa mkoa wa Simiyu kuwa Serikali imetenga shilingi Bilioni 1.5 na wadau wengine wameahidi kutoa shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya kukamilisha wodi ya mama na mtoto.
“Simiyu katika bajeti ya Serikali imetengewa shilingi bilioni 1.5 lakini tumepata pia shilingi bilioni 1.1 kutoka kwa wafadhili kwa ajili ya ujenzi waWodi ya mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu, lengo letu ni kukamilisha ujenzi haraka ili tuiwezeshe Halmashauri ya Mji wa Bariadi, kuchukua majengo ambayo yanatumika sasa hivi kama Hospitali Teule ya mkoa” alisema.
Katika hatua nyingine Waziri Ummy amesema baada ya kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Serikali ina mpango wa kujenga Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Mashariki Mkoani Simiyu, itakayohudumia mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga ili kuipunguzia mzigo Hospitali ya Rufaa ya Bugando ambayo inahudumia mikoa takribani minane.
Ameongeza kuwa pamoja na kuwa na mpango wa kujenga Hospitali ya hiyo Rufaa ya Kanda Simiyu, Serikali imekusudia kujenga Hospitali za Kanda tatu ambazo ni Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini ambayo imeanza kujengwa Mtwara, nyingine itajengwa Tabora(Kanda ya Magharibi ili wananchi wapate matibabu ya kibingwa katika maeneo yao.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha za kujenga jengo hilo, ambazo zitasaidia kuboresha huduma za afya katika mkoa wa Simiyu.
Aidha, Mtaka amesema ardhi kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Mashariki itatolewa bure na akamhakikishia Waziri Ummy ushirikiano wa asilimia 100 kila watakapokuwa wakihitajika kwa namna moja au nyingine ili kufanikisha ujenzi wa hospitali hiyo.
Pamoja na Serikali kuahidi kutoa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa SIMIYU, pia Waziri Ummy amesema Serikali imetenga shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali yaWilaya ya Itilima.
MWISHO
KUPATA PICHA ZA TUKIO HILI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/07/serikali-kutoa-shilingi-bilioni-15.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa