Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini hapa nchini (RITA) unatarajia kuanza kutekeleza mpango wa kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kuanzia mwezi Machi , mwaka huu mkoani Simiyu.
Hayo yameelezwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa RITA, Bi.Emmy Hudson wakati wa Ufunguzi wa semina ya viongozi ngazi ya Mkoa na wilaya iliyofanyika Mjini Bariadi kwa lengo la kuwapa uelewa wa kina viongozi hao juu ya mpango huu utakaotekelezwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Amesema hali ya usajili nchini hairidhishi ambapo amebainisha kuwa, kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 ni asilimia 13.4 tu ya wananchi hapa nchini ndiyo waliosajiliwa na kupewa vyeti vya kuzaliwa.
Ameongeza kuwa ili kuboresha mazingira ya usajili nchini Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) imeandaa mkakati wa maboresho ya kuhakikisha kuwa kila tukio la uzazi linalotokea nchini linasajiliwa kwa wakati, ambao pia unalenga makundi matatu la kwanza likiwa ni la watoto chini ya miaka mitano, kundi la miaka mitano hadi 17 na kundi la miaka 18 na kuendelea.
“Tutakuwa hapa Simiyu kusajili watoto wa umri wa chini ya miaka mitano ambao idadi yao ni 351, 000, takwimu zinaonesha ni asilimia tano tu ya watoto ndiyo waliosajiliwa, kwa hiyo hali ya usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa Simiyu iko chini na ndiyo maana RITA tumeona tuje ili watoto wote wa Simiyu wapate vyeti vya kuzaliwa na kusajiliwa” alisema Kaimu Mtendaji Mkuu RITA.
Amesema RITA itafanya kampeni kwa muda wa wiki mbili za mwanzo ili kuwaandikisha watoto wote ambao walikuwa hawajaandikishwa na kupewa vyeti vya kuzaliwa, baada ya hapo watoto wote watakaozaliwa baada ya hiyo kampeni wataandikishwa katika Ofisi za Watendaji wa Vijiji, Kata na kwenye vituo vya Tiba ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
Aidha, Kaimu mtendaji Mkuu RITA amesema katika kuhakikisha kila mtoto anasajiliwa Serikali imeondoa ada kwa kundi la watoto walio chini ya umri wa miaka mitano hivyo wananchi watapata huduma hii bila malipo yoyote.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema watumishi watakaoshiriki zoezi la usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto chini ya miaka mitano hususani Watendaji wa Kata naVijiji wajengewe uwezo na akaziagiza Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya Mkoani humo kusimamia zoezi hili ili lifanyike kwa ufanisi mkubwa na uzalendo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt.Seif Shekalaghe amesema mpango huu wa usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto chini ya miaka mitano utawasaidia wananchi kupata huduma karibu na maeneo wanayoishi (Ofisi za Watendaji wa Kata na Vijiji) kwa kuwa awali walikuwa wanalazimika kwenda kwenye Ofisi za Wakuu wa Wilaya ili kupata vyeti hivyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Ndg.Abdallah Malela amesema viongozi wa Wilaya watahakikisha kila mtoto anayezaliwa anaandikishwa kupitia Ofisi za Watendaji wa Kata na Vijiji na kupewa cheti, jambo litakalowasaidia kupata takwimu zitakazotumika kufanya maoteo ya wanafunzi wanaopaswa kuanza darasa la kwanza na darasa la awali miaka ijayo.
Kikao hiki kiliwahusisha Wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama Mkoa na Wilaya, Makatibu Tawala Wasaidizi wa Sekretarieti ya Mkoa, Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa na Wilaya, Maafisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya, Waganga Wakuu wa Wilaya, Waratibu wa Huduma za Afya ya mama na mtoto pamoja na watumishi wanaoshughulikia usajili wa vyeti vya kuzaliwa katika Ofisi za Wakuu wa Wilaya.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI JUU YA HABARI HII FUNGUA HAPA:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/02/rita-kuanza-usajili-na-kutoa-vyeti-vya.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa