Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema dhamira ya Kanda mpya ya Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Nane Nane ya Ziwa Mashariki inayojumuisha mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga ni kuwa na Uwanja wa Nanenane utakaofanya Maonesho ya Kilimo Biashara.
Mtaka amesema hayo wakati akifungua kikao cha Maandalizi ya Maonesho ya Nanenane ya Kanda ya Ziwa Mashariki yatakayofanyika katika viwanja vya Nyakabindi kilichowakutanisha Wakuu wa Mikoa mitatu ,Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri na Sekretarieti za Mikoa hiyo, ambacho kilifanyika mjini Bariadi.
Amesema pamoja na kufanya maonesho ya Kilimo Nanenane ambayo huwa yanafanyika kuanzia Agosti Mosi hadi Agosti 08 kila mwaka, kutafanyika Maonesho mengine mara nne kwa mwaka pamoja na matukio mengine yatakayofanyika katika uwanja huo ili kuwe na tija kwa Halmashauri kuwekeza fedha katika uwanja huo.
“Haiwezekani Halmashauri zetu zikawekeza katika uwanja wa NaneNane halafu uwanja uwe unatumika tarehe 01 hadi 08 mwezi wa nane kila mwaka tu, ni lazima tuwe na viwanja ambavyo vitafanya maonesho ya kilimo biashara lakini eneo lile ukiacha maonesho haya ya NaneNane tutafanya maonesho mara nne kwa mwaka” alisema.
Ameongeza kuwa ili kuendana na hali ilivyo sasa ni vema Halmashauri zikakubaliana kujenga jengo la maonesho (exhibition hall) na kuwa na maeneo ya nje kwa ajili ya vipando na mifugo kama ilivyopendekezwa katika vikao vya awali, badala ya kutumia vibanda na mahema kama ilivyozoeleka, ili kuifanya Nane Nane ya Kanda Mpya ya Ziwa Mashariki kuwa ya tofauti.
Katika kikao hicho, Halmashauri 21 za Mikoa ya Mara, Shinyanga na Simiyu zimeagizwa kuwasilisha mchango wa kiasi cha shilingi milioni 20 ndani ya siku saba kwa ajili ya malipo ya awali ya ujenzi wa jengo la maonesho, huku Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Adam Malima akiwataka Wakurugenzi kutelekeleza agizo hilo.
“.....tumekubaliana kuwa kila Halmashauri itatoa shilingi milioni 20 na hili si jambo la masihara, .....ndani ya siku saba tukitoka hapa kila Mkurugenzi atakuja na hundi yake ya shilingi milioni 20, ili itakapofika Juni Mosi haya mambo yakamilike” alisema Malima.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhe. Glorius Luoga ametoa wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote katika mikoa hiyo kuwa wabunifu katika kuhakikisha fedha za kuwezesha ujenzi wa jengo hilo linalotarajiwa kugharimu jumla ya shilingi bilioni 2.1 zinapatikana.
Hivi karibuni Wizara ya kilimo imetangaza Kanda Mpya ya Maonesho ya Nanenane ijulikanayo kama Kanda ya Ziwa Mashariki, ambayo inajumuisha mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga na Uwanja utakaotumika kwa ajili ya Maonesho hayo uko Eneo la Nyakabindi Mjini Bariadi Mkoani Simiyu, ambapo mwaka 2018 Kanda hiyo itakuwa mwenyeji wa maonesho hayo kitaifa.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA KIUNGANISHI HIKI HAPA:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/05/rc-mtaka-tutakuwa-na-uwanja-wa-nanenane.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa