Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametoa wito kwa viongozi kutumia nguvu nyingi kujifunza badala ya kutumia nguvu nyingi kuamua ili wanapofanya maamuzi waamue maamuzi yenye tija kwa maendeleo ya wananchi katika maeneo yao.
Mtaka amesema hayo Machi 11, 2019 Mjini Bariadi katika Mdahalo wa uongozi na maendeleo yenye tija kwa wote uliondaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa viongozi wa Mkoa wa Simiyu,ambao uliwashirikisha viongozi ngazi ya Wilaya na Mkoa.
“Ni vizuri tukatumia nguvu nyingi kujifunza kuliko kuamua kwa sababu kama hutaki kujifunza unataka uamue utaamua hata usiyoyajua, inawezekanaje mtu anateuliwa leo kuwa Mkuu wa Mkoa, Wilaya au Mkurugenzi halafu unakuwa mtaalam wa kila kitu, kilimo wewe, afya wewe, elimu wewe ; unafikiri unaweza kutranform ( kufanya mabadiliko/mapinduzi ya) uchumi wa nani?” alisema Mtaka.
Aidha, katika kumuenzi Mwalimu Nyerere amewaasa viongozi wenzake waliopewa dhamana na Mhe. Rais kuwatumikia wananchi kushughulika na masuala yanayohusu maendeleo ya wananchi badala ya kujikita katika mambo yasiyo na tija ikiwemo ugomvi kati yao.
“Tumeaminiwa na Mhe. Rais tukapewa dhamana tuwatumikie Watanzania wenzetu tujishughulishe na masuala ya wananchi tuache mambo yasiyo na tija kwa wananchi; hivi kuna haja gani DC kugombana na DED au RC kugombana na RAS? Kwa nini tumsumbue Mhe. Rais badala ya kuongelea masuala ya maendeleo ya wananchi abaki kuzungumzia mambo ya ugomvi wa viongozi? Alihoji Mtaka
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Bw. Joseph Butiku ametoa wito kwa viongozi kuheshimu Katibu ya Jamhuri ya Muungano waTanzania na kuishi katika misingi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika uongozi wao.
Aidha, Butiku ametoa rai kwa viongozi wote wa Serikali kutumia madaraka waliyopewa kwa maslahi ya wananchi na wahakikishe wanawafikia wananchi mpaka ngazi za chini ili waweze kuwasaidia namna bora ya kutumia shughuli za uzalishaji wanazozifanya hususani kilimo na mifugo kujikwamua kutoka katika umaskini.
Akitoa mada kwa viongozi wa Mkoa wa Simiyu, Mjumbe kutoka Taasisi ya Mwalimu Nyerere Bw. Gallus Abed amesema katika kuwaletea maendeleo wananchi ni lazima viongozi wajiwekee malengo na kusimamia utekelezaji wa malengo hayo na kuhakikisha wanapima matokeo yake.
Nao baadhi ya Viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakichangia hoja katika mdahalo wa uongozi na maendeleo yenye tija kwa wote wamezungumzia mchango wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere na namna wanavyomuenzi Mwalimu Nyerere katika utekelezaji wa shughuli zao za kuwaletea maendeleo wananchi.
“Tunaishukuru Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa namna ambavyo imeamua kutufikia na kuendelea kutuonyesha, kutukumbusha na kuturejesha ili tuishi maisha ya Mwalimu Nyerere ambaye amekuwa mfano wa kuigwa” Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini.
“Serikali ya awamu ya tano imekuwa ikiyaishi maono ya Baba wa Taifa, Mwl.Julius Nyerere, kama unavyoona Mhe. Rais amekuwa akisema na sisi tunaona miradi mikubwa ya maendeleo inatekelezwa kwa fedha zetu za ndani” Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera.
“Tunatekeleza fikra za Mwalimu Nyerere kwa kuanzia hasa katika utekelezaji wa malengo yaliyoko katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Miaka Mitano kwenye maeneo yetu” Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Bibi.Suzana Sabuni.
MWISHO
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Joseph Butiku katika Mdahalo wa uongozi na maendeleo yenye tija kwa wote uliondaliwa na Taasisi hiyo kwa viongozi wa Mkoa wa Simiyu, ambao ulifanyika Machi 11, 2019 Mjini Bariadi.
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/03/rc-mtaka-viongozi-tutumie-nguvu-nyingi.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa