Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema Mkoa huo unahitaji ushirika imara na wa kisasa unaolenga kuwafikisha wananchi katika Uchumi wa kati.
Mtaka amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Ushirika la Mkoa wa Simiyu uliofanyika katika Ukumbi wa kanisa Katoliki Mjini Bariadi, tukio ambalo limeshirikisha viongozi Serikali na watalaam mbalimbali ngazi ya Mkoa na Wilaya, viongozi wa vyama vya ushirika, Tume ya maendeleo ya Ushirika na wadau mbalimbali wa ushirika.
" Sisi kama mkoa tuko tayari kwa yale ambayo ninyi wenzetu wa Tume ya Ushirika mnadhani kupitia hayo tutakuwa na ushirika imara na utakaoendeshwa kisasa, tuko tayari hata kwa kuwatoa watu wetu kujifunza katika vyama vya ushirika vilivyofanikiwa;ushirika wa Tanzania ukiamua Uchumi wa kati inawezekana"
Aidha, Mtaka amesema wananchi wakielimishwa na kukubali kuungana katika vyama ushirika wanaweza kuondokana na Umaskini, hivyo amesisitiza uwepo wa ushirika imara wenye matokeo chanya katika maeneo muhimu ya uzalishaji, ili hata mikoa mingine ijifunze Simiyu
"Mwalimu Nyerere amewahi kusema namna pekee ya watu maskini kujikomboa ni kuungana, niwasihi wanaushirika kuunganisha nguvu katika ushirika, matajiri wanaungana kuunda makampuni yanayoweza kukopa, yakashtaki na kushtakiwa ninyi unganeni kwenye vyama vya ushirika kujenga uchumi " amesema Mtaka.
Aidha, Mtaka amesema Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB) imekubali kufanya kazi na Mkoa wa Simiyu kwa kuviwezesha vyama vya ushirika na vikundi vilivyosajiliwa kisheria kwa kuwajengea uwezo wanachama na kuwapa mikopo kwa ajili ya kuendesha miradi mbalimbali, hivyo vyama vya ushirika vinapaswa kuchangamkia fursa hiyo.
Akizungumzia mchango wa ushirika katika utekelezaji wa Kauli Mbiu ya Mkoa"Wilaya Moja Bidhaa Moja Kiwanda Kimoja" Mkuu huyo wa Mkoa amesema vyama vya ushirika ndivyo vyenye wazalishaji wa malighafi ya viwanda, hivyo jukwaa la ushirika litumiwe vizuri katika kuweka mikakati ya kuimarisha vyama vya ushirika na Viongozi wa Serikali wako tayari kuonesha ushirikiano.
Katika hatua nyingine Mtaka amesema mkoa unaandaa andiko linalolenga kuwakusanya wakulima na wanaushirika wote pamoja, ambapo watatumia vyumba vya madarasa katika Shule za Serikali wanafunzi watakapokuwa likizo kupewa mafunzo ya ushirika na kilimo na Wataalam wa Halmashauri, Mkoa na Chuo Kikuu cha Ushirika, ili kuimarisha ushirika na kuongeza tija katika kilimo na mifugo.
Sanjali na hilo Mtaka amesisitiza kuwa mkoa wa Simiyu ndio unaoongoza kwa kulima pamba hapa nchini, hivyo ni vema kukawa na ushirika wenye kuleta majawabu kwa changamoto zinazowakabili wakulima wa pamba kuondoa kero kwa wakulima na kuongeza ubora katika uzalishaji.
Kwa Upande wake Kaimu Naibu Mrajis kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Ndg.Collins Nyakunga amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kwa kuonesha nia ya kuimarisha ushirika katika mkoa huo na kuona kuwa kupitia ushirika wananchi wanyonge wanaweza kutatua matatizo yao ya kiuchumi na Kijamii.
Nyakunga amesema Tume ya Maendeleo ya Ushirika itaandaa namna ambayo itautoa ushirika katika uendeshaji wa kizamani uendeshwe kisasa, tafiti zitafanyika kupitia Chuo Kikuu cha Ushirika kuona namna ya kuongeza bei, thamani ya zao la pamba na ushirika mkoani Simiyu kuimarika.
Naye Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Simiyu, Ndg Mathias Shineneko amesema Mkoa huo umejiwekea mkakati wa kuakikisha vyama vya ushirika vinajielekeza katika kuweka taratibu za kuongeza na kuimarisha mitaji, hisa na akiba ili kujiimarisha kiuchumi.
Wakati huo huo Ezekiel Ganji kutoka Chama cha Msingi Sola wilayani Maswa ameiomba Serikali kuwashirikisha wakulima wa pamba katika maamuzi ya kupanga bei badala ya kupangwa na makampuni yanayonunua pamba na kusisitiza kuwa katika ukaguzi wa vyama vya ushirika Serikali iangalie uwezo wa vyama hivyo na kupunguza tozo za ukaguzi kwa kuwa vyama vingi havina uwezo mzuri kifedha
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa