Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewataka wadau na mashirika mbalimbali wanaofanya kazi na Mkoa huo katika sekta ya Afya kuelekeza fedha zao zaidi katika masuala yanayojibu mahitaji ya wananchi wa Mkoa huo kwenye Afya badala ya kujikita zaidi katika kugharamia mafunzo na semina kwa watumishi.
Mtaka ameyasema hayo katika kikao kilichofanyika Februari 26, Mjini Bariadi kwa lengo la kufanya tathmini ya mchango wa fedha za wahisani na wadau mbalimbali wa sekta ya Afya mkoani Simiyu na matokeo yake katika mahitaji halisi ya Kiafya kwa wananchi.
Mtaka amesema mkoa huo una wadau wengi wanaounga mkono juhudi za Serikali katika sekta Afya na wanatoa fedha nyingi ambazo zikiwekwa pamoja na fedha zinazotengwa na Serikali kupitia bajeti za Halmashauri zinaweza kujibu mahitaji ya mkoa huo ambayo ni pamoja na upungufu wa zahanati na vituo vya Afya
“ Msingi mkubwa wa kikao hiki ni kutaka tufanye tathmini ya fedha zinazotolewa na wadau ndani ya mkoa wetu, kwa mwaka huu kwenye Halmashauri zetu tumetenga Bilioni 33.4 na tuna shilingi bilioni 11 kutoka kwa wadau kwa ajili ya sekta ya afya, hivi ‘impact’(matokeo) ya hizi bilioni 11 iko wapi? Natamani hapa kila mwenye fedha yake atuambie mwaka huu atafanya nini” alisema Mtaka.
“Nashukuru TAMISEMI mko hapa hili ni la kuliangalia , kama tunaingia mikataba ya shilingi bilioni 11 kwa mwaka na mashirika yanayofanya kazi za Afya ndani ya Mkoa kwa ajili ya kuwajengea uwezo watumishi, uhamasishaji na semina, wakati tukiwa kwenye mazingira ambayo hatuna hata nusu ya idadi ya zahanati na vituo vya afya vinavyohitajika ni lazima tutafakari wote” alisisitiza Mtaka.
Wakati huo huo Mtaka ametoa wito kwa wataalam wa Afya kuendelea kutoa elimu na kuwahamasisha wananchi kuzingatia uzazi wa mpango na akasisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa wazazi watarajiwa (vijana) ili waanze kufanya maandalizi mapema juu ya maamuzi ya idadi ya watoto watakaoweza kuwahudumia baadaye.
Naye Katibu Tawala Mkoa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini amesema malengo waliyojiwekea katika kikao hicho ni pamoja na kuhakikisha kazi zinazofanywa na wadau wa Afya mkoani humo zinajibu matatizo ya Wanasimiyu na namna ya kuwa na uratibu mzuri wa shughuli zao, mambo ambayo yamepokelewa na wadau hao na kuahidi kuweka uratibu mzuri ili kuimariasha afya za wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirikala Cuso International Tanzania, Ndg.Romanus Mtung’e amesema wadau wa Afya Mkoani humo watashirikiana na Viongozi na Wataalam wa Afya katika kuweka mipango ya baadaye na watazingatia vipaumbele ambavyo vitaleta matokeo chanya yanayoonekana kwa wananchi mkoani humo.
Kikao cha wadau wa Afya na Viongozi Mkoa Simiyu kimewahusisha Viongozi na Wataalam wa Afya ngazi ya Mkoa na Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Wilaya, Viongozi wa Dini pamoja na wadau(mashirika) wa Afya wanaofanya kazi na mkoa wa Simiyu wakiwemo AMREF, AGPAHI, CUAMM, UNFPA, Mkapa Foundation, AMERICARE, PSI,Red Cross, ICAP, TAMA, INTRAHELTH, WORD VISION, BORESHA AFYA, CHAI, MARIESTOPES na BRIDGE2 AID.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA HAPA:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/02/rc-mtaka-fedha-za-wadau-wa-afya-zilenge.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa