Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka na Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo la Kusini mwa Tanzania, Mark Malekana,wametoa salamu za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongela, wananchi wa Mwanza pamoja na familia na ndugu wa waliopoteza maisha katika ajali ya kuzama kwa Kivuko cha MV Nyerere iliyotokea Septemba 20, 2018 huko Ukerewe Mwanza.
Wakitoa salamu hizo kwa nyakati tofauti Septemba 22, 2018 wakati wa kufunga makambi ya Waadiventista Wasabato katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu, Mhe. Mtaka na Askofu Malekana wamewaombea majeruhi wote wapone haraka na kurejea katika majukumu yao.
Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Simiyu amasema msiba huo mkubwa umewagusa watu wengi ikiwepo mkoa wa Simiyu ambapo mwalimu mmoja kutoka katika Kata ya Kalemela wilayani Busega amepoteza maisha katika ajali hiyo.
“Mkoa wa Simiyu katika wilaya ya Busega mwalimu wetu mmoja wa Shule ya msingi katika kata ya Kalemela, Mwalimu Mtaki amefariki kwenye ajali hii alikuwa anaenda kusalimia wazazi wake, huu ni msiba ambao umegusa maeneo mengi”
“ Kwa niaba ya wananchi wote wa mkoa wa Simiyu tunatoa salamu za pole kwanza kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongela, wananchi wa Mwanza lakini zaidi pole kwa familia ambazo zimeguswa na jambo hili, tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu marehemu wote na wale ambao wamenusurika Mungu aendelee kuwaimarisha wapone haraka” alisema Mtaka
Ameongeza kuwa Viongozi wa Mkoa wa Simiyu siku ya Jumapili tarehe 23 Septemba, 2018 wataungana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, viongozi wa Mkoa wa Mwanza, viongozi wengine wa Serikali katika tukio la kuwahifadhi waliopoteza maisha katika ajali hiyo.
Naye Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo la Kusini mwa Tanzania, Mark Malekana amesema “Kwa niaba ya Kanisa la Waadventista Wasabato na washiriki wote napenda kutoa salamu za pole kwanza kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongela, wananchi wa Mwanza kwa msiba huu mzito ulioleta majonzi kwetu Watanzania”
“Kanisa pia linatoa pole kwa familia zilizoguswa na ajali hii na ni ombi la kanisa kwamba wale ambao walijeruhiwa Mungu awapatie uponyaji wa haraka na wale ambao wamelala ambao waliweka maisha yao kwa Yesu, ahadi ni kwamba Yesu atakapokuja mara ya pili atawaita kutoka makaburini” alisema Askofu Malekana
Ameongeza kuwa Kanisa linaungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, viongozi wengine na wananchi kuomba utulivu na mshikamano wakati huu wa majonzi.
MWISHO.
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/09/rc-mtaka-askofu-kanisa-la-sda-watoa.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa