Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka amezishauri taassi zinazosimamia masuala ya biashara kuwajengea uwezo wafanyabiashara ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha umuhimu wa kusajili kampuni zao hatua itakayowawezesha kuendesha shughuli zao kwa tija.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kampeni ya kitu bomba inayoendeshwa na kampuni ya simu ya Haloteli mjini Bariadi,Mtaka amesema ili kuwawezesha wafanyabiashara kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ni muhimu kuandaa mfumo utakaowatambua kuanzia ngazi ya chini hatua itakayosaidia kufuatilia mienendo yao ya kibiashara ikiwemo kuchangia pato la mkoa na taifa kwa ujumla.
“Nawapongeza sana Halotel kwa hatua hii ya ubunifu mliyotuonyesha, ninaamini huu ni mwanzo mzuri kwenu wa kubuni huduma nyingine muhimu zitakazowasaidia wafanyabiashara na makundi mengine muhimu katika maeneo mbalimbali”.
“Kwa upande wetu Simiyu, sisi ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa mifugo mingi nchini halikadalika ni mkoa unaoongoza kwa kilimo cha pamba, hivyo tungefurahi sana endapo Halotel mngekuja na vifurushi vitakavyogusa maeneo hayo ,” alisisitiza Mtaka.
Aidha Mtaka ameishauri kampuni ya simu ya Halotel kuweka utaratibu utakaowawezesha kujitathmini mara kwa mara ili kujua nguvu ya soko lake na mahitaji ya ziada ya wateja wake hatua itakayoiwezesha kuhimili ushindani na kuwa miongoni mwa kampuni zinazoendesha biashara zake kwa kuzingatia mahitaji ya wateja wake.
Halikadhalika Mhe Mtaka ameiagiza kampuni ya Godtech kuhakikisha inawaelimisha wajasiliamali wadogo mkoani Simiyu umuhimu wa kumiliki na kusajili biashara zao kupitia mfumo rasmi ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali.
“ Naendelea kusisitiza Simiyu tumejiandaa kuendesha biashara zetu kimkakati, ili kutekeleza adhma hii kwa vitendo, wafanyabiashara wetu wataendelea kufanya biashara saa 24, lakini pia ninakuagiza mheshimiwa DC fungeni taa sokoni kuruhusu biashara zifanyike mpaka saa nne usiku”, aliongeza RC Mtaka.
Kwa upande wake balozi wa kapeni ya Kitu bomba ambaye pia ni msanii maarufu wa filamu nchini Jackob Stephen maarufu kama JB ameahidi kuzitangaza kikamilifu fursa zinazopatikana mkoani Simiyu kupitia kampeni hiyo huku akiwataka vijana wenye vipaji kuitumia nafasi hiyo kukuza vipaji vyao.
Uzinduzi wa kampeni hiyo ya Kitu Bomba inayolenga kuwajengea uwezo wananchi katika kupambana na umasikini iliyozinduliwa mjini Bariadi umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara na wadau wa maendeleo.
Mwisho
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa