Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amepiga marufuku wakopeshaji wanaowakopesha walimu, kushikilia kadi zao za kutolea fedha benki (ATM) na vyeti vya taaluma kama dhamana ya mkopo.
Mtaka ametoa marufuku hiyo wilayani Itilima wakati wa hafla ya kuwapongeza walimu kwa kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa mwaka 2019.
“Walimu jiepusheni na mikopo isiyo na ulazima, benki yenu ipo itumieni; imefika wakati walimu wanaweka kadi zao za ATM kama dhamana wengine wanaweka mpaka vyeti vya taaluma; hii biashara hapana, kitambulisho cha benki na vyeti ni mali mwalimu,”alisema Mtaka.
Aidha, amewapongeza walimu kwa kazi nzuri wanayofanya na kuwaeleza kuwa wana nafasi kubwa ya kuufanya mkoa kufanya vizuri zaidi katika mitihani yote ya Kitaifa ambapo ameeleza kuwa lengo la Mkoa ni kutoka kwenye nafasi kumi bora na kushika nafasi tatu bora kwa mitihani yote ya Kitaifa kwa shule za msingi na sekondari.
Katika hatua nyingine Mtaka ameendelea kusisitiza utekelezaji wa agizo la walimu kupewa kiupaumbele kuhudumiwa katika taasisi za Umma ili wapate muda wa kwenda kuwafundisha wanafunzi wanaowaacha shuleni wakati wanapoenda kupata huduma.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wialya ya Itilima, Bi. Elizabeth Gumbo amesema hali ya ufaulu katika Halmashauri hiyo imekuwa ikipanda kila mwaka, kutoka asilimia 56.2 mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 78.52 mwaka 2019.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini ametoa wito kwa walimu na wadau wengine wa elimu kutekeleza mkakati wa elimu wa mkoa kila mmoja kwa nafasi yake ili mkoa uweze kufikia lengo la kuwa miongoni mwa mikoa mitatu bora.
Mbunge wa Jimbo la Itilima, Mhe. Njalu Silanga amewapongeza walimu kwa kazi nzuri waliyofanya na kuahidi kuwa Wilaya hiyo itaendela kufanya vizuri kimkoa na Kitaifa huku akieleza mpango wa Wilaya ya Itilima kuwa ni kuhakikisha kila shule ya sekondari wilayani humo inakuwa na bweni.
Nao walimu wa Wilaya ya Itilima wamesema kuwa wataendelea kufanya kazi kwa bidii huku wakiahidi kutekeleza ikakati yote inayowekwa katika ngazi ya Mkoa, wilaya mpaka ngazi ya shule ili waweze kufikia azma ya kuufikisha mkoa katika mikoa tatu bora nchini katika mitihani yote ya Kitaifa.
“Kutokana na mikakati ambayo mkoa umeweka ukiwemo wa kambi za kitaaluma na wanafunzi kupata chakula cha machana shuleni itasaidia sana kuinua ufaulu kwa shule za msingi na sekondari,” alisema mwalimu Bindi Busagala.
Shule na walimu waliofanya vizuri katika mitihani ya Kitaifa wamepewa zawadi ya vyeti na fedha taslimu.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2020/03/rc-mtaka-apiga-marufuku-watoa-mikopo.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa