Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka amemkabidhi Mwenge wa Uhuru Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Zainab Taleck na kumhakikishia Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018 Ndg. Charles Kabeho kuwa atachukua hatua dhidi ya mapungufu yaliyobainika wakati Mwenge wa Uhuru ukipitia baadhi ya miradi ya maendeleo mkoani Simiyu.
Mtaka amesema ushauri na mapendekezo yaliyotolewa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018 Ndg. Charles Kabeho yatafanyiwa kazi,ikiwa kuna mahali pa kuchukua hatua, hatua stahiki zitachukuliwa na ikiwa kuna mahali pa kufanya maboresho ili miradi hiyo itekelezwe katika viwango vinavyokidhi haja ya kutoa huduma kwa wananchi, Serikali ya mkoa itahakikisha inasimamia.
“Ndugu Kiongozi wa Mbio za mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018 na wakimbiza Mwenge wenzako, tunawashukuru kwa kuwa sehemu ya jicho la tatu kwenye miradi inayotekelezwa ndani ya mkoa, niwahakikishie kwamba tutachukua stahiki pale ambapo palionesha ukakasi kwenye taarifa zetu na pale ambapo mliona kunahitajika hatua ili miradi iweze kufanya kazi kwa ufanisi katika kutoa huduma kwa wananchi tutachukua hatua”
Kwa upande wake Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2018 Ndg. Charles Kabeho amewashukuru viongozi na wananchi wa Mkoa wa Simiyu kwa ushirikiano waliompa yeye na wakimbiza Mwenge wenzake walipokuwa Simiyu.
Aidha, Kabeho alitoa rai kwa watumishi wa Umma kuachana na kufanya kazi kwa uzembe na mazoea badala yake wafanye kazi kwa weledi na bidii, hususani katika usimamizi wa miradi ili iweze kutekelezwa kwa wakati katika viwango vya ubora unaotakiwa na wananchi wapate huduma kwa wakati.
Mwenge wa Uhuru umekabidhiwa katika kijiji cha Wishiteleja katika Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga ambapo ukiwa mkoani Simiyu ulipitia miradi 36 yenye thamani ya shilingi bilioni 8.4.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa