Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amesema ushiriki katika michezo kwa watumishi ni moja ya njia za kuongeza ari ya utendaji kazi katika maeneo yao.
Sagini ameyasema hayo mwishoni mwa wiki Novemba 10, 2018 jioni wakati akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu na Walimu wa Manispaa ya Musoma mkoani Mara mara baada ya kumalizika kwa mechi ya kirafiki kati ya watumishi hao iliyochezwa katika Uwanja wa Posta Mjini Musoma, ambapo wenyeji Timu ya Walimu walikubali kichapo cha goli nne kwa tatu kutoka kwa Timu ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.
“Mtu aliye na mwili wenye afya, akili yenye afya, aliye na uwezo wa kuruka na kuwepa ngwala kama nilivyokuwa nawaona hapa ni lazima hata katika kazi zake atafanya vizuri” alisema Sagini.
Aidha, Sagini ametoa wito kwa Maafisa Masuuli katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kuwaunga mkono watumishi wao katika masuala ya michezo kwa kuwezesha wanapohitaji msaada kwao hususani katika suala la kuwawezesha kifedha, ili waweze kushiriki michezo mbambali ambayo pia inawasaidia kuimarisha afya zao na kuwaepusha na magonjwa yasiyoambukiza.
Akitoa shukrani kwa Timu ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Timu ya Walimu Manispaa ya Musoma kucheza mchezo huo kwa nidhamu ya hali juu, Afisa Michezo wa Mkoa wa Mara, Bw. Evance Sangawe amesema nidhamu iliyooneshwa ni ishara kwamba watumishi hao wa Umma wanaweza kufanya kazi kwa kujituma bila kusimamiwa.
Kwa upande wake Kocha Msaidizi wa Timu ya Walimu wa Manispaa ya Musoma, Mwl. Yisambi Mwazembe amesema mechi za kirafiki zina umuhimu mkubwa kwa watumishi wa umma kwani zina nafasi kubwa ya kuwakutanisha watumishi ambao walioachana muda mrefu shuleni, vyuoni na hata katika maeneo mengine ya kazi zao.
Naye Nahodha wa Timu ya Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Elias Sebastian amesema mechi hiyo ya kirafiki imewakutanisha na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu na watumishi wa Manispaa ya Musoma ambao hawajawahi kuonana hapo awali, hivyo imechangia watumishi hao kufahamiana na wenzao.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KATIKA TUKIO HILI FUNGUA HAPA:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/11/ras-simiyu-ushiriki-wa-michezo-kwa.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa