Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga ametoa wito kwa viongozi wa dini na waganga wa tiba asili mkoani Simiyu kushirikiana na Serikali katika juhudi mbalimbali za kupunguza vifo vya wakina mama wajawazito na watoto vitokanavyo na uzazi.
Mmbaga ameyasema hayo katika kikao chake na viongozi wa dini na waganga wa tiba asili wilayani Itilima, kilichofanyika jana Februari 26, 2021 katika makao makuu ya wilaya hiyo Lagangabilili.
“Sisi kama mkoa tunasema hatutaki kuona mwanamke yeyote anapoteza maisha wakati akijifungua na mtoto akipoteza maisha wakati anazaliwa tunasema waliokufa sasa basi, ni muhimu viongozi wa dini na waganga wa jadi wakashirikiana na Serikali katika kueleimisha jamii juu ya umuhimu wanawake wajawazito kupata huduma stahiki za afya kwa wakati, tunajua haya makundi yanakutana na yanawahudumia watu wengi,” alisema Mmbaga.
Aidha, Mmbaga amesema Serikali inatambua mchango na kazi nzuri inayofanywa na viongozi wa dini kupitia kamati za amani huku akisisitiza kamati hizo ziendelee kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazokutana na taasisi wanazozisimamia (madhehebu ya dini).
Wakati huo huo Mmbaga ametoa rai kwa waganga wa tiba asili mkoani Simiyu kuchagua viongozi waadilifu watakaowaunganisha pamoja na kuwa msaada kwao katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, miongozo, kanuni na taratibu za nchi zilizowekwa.
Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe. Benson Kilangi amewapongeza waganga wa tiba asili kwa kuwa wadau muhimu wa maendeleo katika wilaya hiyo kwa kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa, kutoa chakula kwa ajili ya wanafunzi wanaokuwa katika kambi za kitaaluma; huku akiwaomba waimarishe umoja wao na kuwa na uongozi imara ili waweze kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili.
Mchungaji wa Kanisa la EAGT Lagangabilili ameomba Serikali ione uwezekano wa kuunda chombo kitakachowasaidia viongozi wa dini na waganga wa tiba asili ili makundi hayo yaweze kutekeleza majukumu yao kwa misingi ya sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayotolewa na serikali, huku Padri Ivo Komba akitoa wito kwa viongozi wa dini kuwaongoza waumini wao katika imani ya kweli iliyo thabiti mbele za Mwenyezi Mungu.
Kwa upande wake Bw. Tandala Shuri Mganga wa asili kutoka kata ya Nkoma ameomba waganga wa tiba asili washirikiane na viongozi wa dini kufanya kazi kwa kufuata taratibu huku akieleza kuwa baadhi ya waganga wa tiba asili siyo waaminifu wamekuwa wakikiuka taratibu zilizowekwa hivyo akaiomba serikali isisite kuwachukulia hatua waganga wote watakaokwenda kinyume cha sheria zilizopo.
“Tunaomba serikali ishughulike na waganga wahalifu na sisi waganga ndiyo tuwe mstari wa mbele kuwafichua wahalifu hao ili uhalifua wao usituchafue waganga wote, tufuate utaratibu unatakiwa na serikali katika kufanya kazi zetu tusitafute kugombana na serikali,” alisema Tandala Shauri.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Dkt. Anold Musiba amesema waganga wote wanapaswa kuomba leseni za kuendesha shughuli zao ili waweze kutambulika kisheria ambapo mpaka sasa jumla ya waganga wa tiba asili 1387 wametambuliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Itilima.
Aidha, Dkt. Musiba ametumia fursa hiyo kuwaomba waganga hao kuwaelekeza wakina mama wajawazito, wakina mama wenye watoto wenye utapiamlo mkali na matatizo yote ya lishe kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya mapema.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2021/02/ras-simiyu-awaasa-viongozi-wa-dini.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa