Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Bw. Anderson Njiginya kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa majengo ya upasuaji na wodi ya wazazi katika Hospitali ya Wilaya ili kuboresha hali ya utoaji wa huduma kwa wananchi katika hospitali hiyo.
Mmbaga ametoa agizo hilo Septemba 09, 2020 wakati zoezi la usimamizi shirikishi alipotembelea hospitali hiyo kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo hayo ambayo yanapaswa kukamilika na kuanza kutoa huduma ifikapo Septemba 30, 2020.
“Nampongeza Mkurugenzi kwa kujiongeza, badala ya kusubiri kibali kutoka HAZINA kulipa fedha za kukamilisha ujenzi wa majengo haya, amejiwekea utaratibu wa kuwalipa mafundi wetu, nimeelekeza kuwa aongeze kiwango anachotoa kwa kila juma ili kuongeza kasi ya ujenzi na hatimaye majengo haya yaweze kukamilika na kutumika kwa huduma kusudiwa,” alisema Mmbaga.
Aidha, Mmbaga ameongeza kuwa ukamilishaji wa majengo hayo uende sambamba na utunzaji wa mazingira ambao utajumuisha upandaji miti, bustani za maua na utunzaji wa miti asili huku akitoa pongezi kwa Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri hya Wilaya ya Busega kwa usimamizi mzuri katika ujenzi wa hospitali hiyo na kumuagiza Mkurugenzi kumthibitisha katika cheo chake.
Wakati huo huo Mmbaga ameelekeza Timu ya usimamizi wa afya ngazi ya wilaya (CHMT) kuimarisha usimamizi katika mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) uliboreshwa hususani watoa huduma ngazi ya jamii wanaohusika katika usajili ili wananchi waweze kupata huduma zilizokusudiwa na serikali.
Katika hatua nyingine Mmbaga ametembelea kikundi kinachojihusisha kilimo cha umwagiliagi kilichopo kijiji cha Chamgasa na kuelekeza wataalam wa fedha na uchumi waweze kutoa elimu kwa wakulima hao juu ya utunzaji na matumizi ya fedha ili wanapopewa mikopo na wadau waweze kutekeleza miradi ambayo itakuwa endelevu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Bw. Anderson Njiginya amesema atahakikisha fedha zinatolewa kwa wakati kwa mafundi wanaoendelea na ujenzi wa majengo ya Upasuaji na wodi ya wazazi katika hospitali ya wilaya ili shughuli za ujenzi zisikwame.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt. Khamis Kulemba ameipongeza Timu ya usimamizi wa afya ngazi ya wilaya (CHMT) kwa namna inavyotekeleza majukumu yake huku akisisitiza watumishi wote wa afya kuendelea kutoa huduma stahiki kwa wananchi.
Nao baadhi ya watumishi wa afya katika kituo cha afya Lukungu wameomba miundombinu katika vituo vya kutolea huduma za afya iboreshwe ili kutoa huduma kulingana na hadhi za vituo hivyo na wananchi wapate huduma wanazotarajia kuzipata katika vituo husika.
MWISHO.
KUPATA PICHA ZAIDI TAFADHALI TEMBELEA BLOGU YETU YA MKOA KUPITIA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2020/09/ras-simiyu-ataka-majengo-ya-upasuaji.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa