Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini amewataka Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri Mkoani humo kuandaa mipango mikakati katika Halmashauri zao.
Sagini ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya uandaaji wa Mipango mikakati ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Mkoani humo yanayofanyika Lamadi wilayani Busega, chini ya Mpango wa Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma katika Mamlaka za Serikali za Mitaa(PFMRP).
Amesema wakurugenzi wote wahakikishe wanatumia rasilimali zilizopo katika maeneo yao kuhakikisha kuwa wanakamilisha uandaaji wa mipango mikakati hiyo.
“ Niwaombe Wakurugenzi Watendaji kuepuka visingizio vya kutokuwa na fedha kutekeleza jambo hili na badala yake mjipange kwa kutumia rasilimali tulizonazo” amesema.
Aidha, amesema Mpango Mkakati ni muhimu kwa kila Halmashari kwa kuwa unasaidia Halmashauri kufikia malengo ya kuanzishwa kwake na kuboresha utoaji huduma za kiuchumi na kijamii kwa wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Ndg.Abdallah Malela amesema mafunzo hayo yatawasaidia wao kama viongozi na watendaji wengine katika Halmashauri zao kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo zikiwemo za uanzishwaji na uendeshaji wa viwanda kimkakati.
Wakati huo huo pia Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuendelea kutenga maeneo ili kuwezesha utekelezaji wa Sera ya Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda Mkoani humo.
Mafunzo ya uandaaji wa Mipango mikakati ya Mamlaka za Serikali za Mitaa (Halmashauri) Mkoani yamewahusisha Wakurugenzi, Wataalam wa Idara ya Kilimo, Fedha, Mipango na Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri zote sita (06) za mkoa huo (Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Busega, Itilima, Maswa, Meatu na Halmashauri ya Mji Bariadi).
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa