Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Ekwabi Mujungu amewataka wanafunzi walimu na maafisa elimu walio katika kambi ya Michezo ya UMITASHUMTA Ngazi ya mkoa kudumisha nidhamu wakati wote watakapokuwa katika kambi hiyo ili Mkoa uweze kufanya vizuri katika michezo na elimu kwa ujumla.
Mujungu ameyasema hayo Juni 12, 2019 wakati akifungua Mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya Mkoa katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa, ambayo kwa mwaka 2019 yanaongozwa na Kauli Mbiu “MICHEZO NA SANAA KWA ELIMU BORA PIA NI AJIRA”.
“Ili tuweze kufanya vizuri katika michezo na Elimu kwa ujumla napenda kusisitiza nidhamu ya usimamizi wakati wa mashindano, kambi na ngazi ya Taifa; ni lazima kuwe na nidhamu binafsi kwenu ninyi wachezaji na wasimamizi wanaowasimamia, kama hakuna nidhamu tusitarajie matokeo mazuri” alisema Mujungu.
Aidha, Mujungu ametoa wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri mkoani hapa kuwawezesha Walimu wa michezo kupata mafunzo ili waweze kujua vema sheria za michezo mbalimbali kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi kufahamu michezo hiyo na kuamua michezo hiyo kwa haki.
Katika hatua nyingine ametoa wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya michezo ikiwa ni pamoja na upungufu wa miundombinu ya viwanja, walimu wa michezo na ratiba ya michezo kutofuatwa.
Awali akitoa taarifa ya mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya Mkoa mwaka 2019, Kaimu Afisa Elimu wa mkoa, Mwl. Onesmo Simime amesema mashindano hayo yatashirikisha michezo ya aina sita ambayo ni riadha, mpira wa miguu, mpira wa wavu, mpira wa mikono, mpira wa pete(wavulana na wasichana kwa michezo yote mitano) na fani za ndani.
Kwa upande wake Kaimu Afisa michezo wa Mkoa, Bw. Charles Maganga amesema kupitia mashindano haya ya UMITASHUMTA mwaka 2019 Walimu kwa kushirikiana na Maafisa Michezo waliopo kambini watahakikisha wanachagua wachezaji wazuri watakaounda timu ya Mkoa yenye ushindani na matarajio yao ni kufanya vizuri katika mashindano ya Kitaifa.
Naye mwanamichezo (mwanafunzi) Jeremia Boniface Jeremia kutoka Halamshauri ya Wilaya ya Bariadi akizungumza kwa niaba ya wenzake amesema matarajio yao ni Mkoa wa Simiyu kufanya vizuri kwa kuwa wameandaliwa vizuri na kaahidi kuwa watakuwa na nidhamu wakati wote wa mashindano hayo.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/06/nidhamu-yatajwa-kuwa-msingi-wa.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa