Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI ametoa miezi miwili kuanzia sasa kwa Wakurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi na Itilima kukamilisha ujenzi wa mabweni katika shule ya sekondari Bariadi, Nyasosi na Itilima ili wanafunzi waliokusudiwa kukaa katika mabweni hapo wapate huduma tarajiwa kwa wakati.
Silinde ametoa agizo hilo wakati alipotembelea shule hizo wakati wa ziara yake Machi 05, 2021 Mkoani Simiyu yenye lengo la kukagua ujenzi wa majengo ya miundombinu ya elimu ikiwemo mabweni, mabwalo na vyumba vya madarasa.
Amesema Serikali haitatoa fedha nyingine kukamilisha mabweni, mabwalo na madarasa ambayo bado hayajakamilika na haitakubali yabaki magofu hivyo ni jukumu la Halmashauri husika kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha majengo hayo ili wanafunzi waliokusudiwa kutumia wapate haki yao.
“Nimeridhishwa na kiwango cha ujenzi wa madarasa na thamani ya fedha inaonekana ninawapongeza sana, kuhusu mabweni mhakikishe yanakamilika na ninaahidi kurudi tena hapa mwezi Mei kuja kukagua kuona namna mlivyotekeleza, yasipokamilika ninawaambia wazi nitawavua madaraka wakuu wa shule na maafisa Elimu sekondari,” alisema Silinde.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Bi.Elizabeth Gumbo ameahidi kukamilisha ujenzi wa bweni shule ya sekondari Itilima ifikapo Aprili 30, 2021 huku Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Bw. James John akiahidi kukamilisha bweni la Shule ya sekondari Nyasosi tarehe hiyo hiyo na Mkurugenzi wa Mji wa Bariadi,Melkizedeck Humbe ameahidi kukamilisha ujenzi Mei 15, 2021.
Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe.Benson Kilangi amesema shule ya Sekondari Itilima ilipokea shilingi milioni 80 kwa ajili ya ujnezi wa bweni ambapo amebainsha kuwa baadhi ya sababu zilizopelekea mradi huo kutokamilika kwa fedha hiyo ni pamoja na aina ya udongo uliopo katika eneo la Ujenzi kuhitaji msingi mrefu na imara uliotumia fedha nyingi tofauti na makadirio pamoja na kupanda kwa bei za vifaa vya ujenzi.
Pamoja na changamoto hizo Kilangi amesema Serikali wilayani humo itahakikisha Bweni la Shule ya Sekondari Itilima linakamilika kwa wakati ili kuwawezesha wanafunzi kupata huduma iliyokusudiwa kwao.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe. Festo Kiswaga amewaagiza wataalam wa Halmashauri zote mbili za Wilaya ya Bariadi kuhakikisha wanakamilisha majengo yote yaliyoletewa fedha na serikali huku akimhakikishia Naibu Waziri kuwa mabweni ya Bariadi sekondari na Nyasosi sekondari yatakamilika kwa wakati.
Katika hatua nyingine Kiswaga amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya hiyo kumpelekea taarufa ya fedha zote za miradi zinazoingia ili kamati ya ulinzi na usalama iweze kujua na kuweka utaratibu wa kuzisimamia na kuhakikisha zinatekeleza miradi kulingana na maelekezo ya Serikali.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2021/03/naibu-waziri-silinde-atoa-miezi-miwili.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa